Dereva basi la Isamilo afariki akiwa safarini

Muktasari:

Dereva wa Basi la Isamilo linalofanya safari zake kutoka Mwanza kwenda Mbeya nchini Tanzania Sebastian Mathias (43) mkazi wa Mwanza amefariki akiwa njiani kutoka Mbeya kwenda Mwanza. Mwili wake umehifadhiwa kituo cha afya Tinde mkoani Singida.

Shinyanga. Dereva wa Basi la Isamilo linalofanya safari zake kutoka Mwanza kwenda Mbeya nchini Tanzania Sebastian Mathias (43) mkazi wa Mwanza amefariki dunia wakati akiendelea na safari kutoka Mbeya kwenda Mwanza.                      

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga, Deborah Magiligimba amesema tukio hilo limetokea leo Ijumaa Machi 20,2020 saa nne asubuhi.

Kamanda Magiligimba amesema Sebastian wakati akitoka Mbeya kwenda Mwanza alikuwa akijisikia vibaya walipofika Singida ndipo hali yake ilibadilika wakawa wamebadilishana na dereva mwenzake.

“Katika basi hilo, madereva walikuwa wawili lakini baada ya kuona hali yake imebadilika alibadilishana na mwenzake yeye akaendelea kupumzika lakini walipofika saa nne asubuhi akawa amezidiwa sana, wakambeba na kumpeleka katika kituo cha afya Tinde," amesema Kamanda Magiligimba.

Magiligimba amesema baada ya kumfikisha hospitali daktari alibaini kuwa tayari Sebastian alikuwa ameshafariki dunia.

Amesema kwa kuwa gari lina madereva wawili, dereva mwingine ameendelea na safari kwenda Mwanza na maiti imehifadhiwa katika kituo cha afya cha Tinde.