Dereva lori la mafuta lililoteketea kwa moto apatikana akiwa hai

Muktasari:

Polisi mkoani Ruvuma nchini Tanzania limesema dereva wa lori lililokuwa limebeba shehena ya mafuta ya petroli lililopata ajali kisha kichwa cha gari hilo kuteketea kwa moto amepatikana akiwa hai.

Songea. Hubert Mtete ambaye ni dereva wa lori lililokuwa limebeba shehena ya mafuta ya petroli lililoacha njia na kugonga mti Kijiji cha Hangangadinda mkoani Ruvuma nchini Tanzania kisha kichwa cha gari hiyo kuwaka moto na kuteketea amepatikana akiwa hai.

Polisi mkoani humo kwa kushirikiana na wananchi walikuwa wakimtafuta dereva huyo mwenye umri kati ya miaka 37-40 kujua kama yuko hai au aliteketea katika ajali hiyo iliyotokea juzi Jumapili Agosti 11,2019

Gari aina ya Scania yenye namba za usajili T243 DTV ikiwa na shehena ya mafuta ya petrol lita 33,000 mali ya James Mwinuka ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Njombe Filling station ikitokea Njombe kwenda Songea ilipata ajali huku tenki likisalia pasina kuungua

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Simon Marwa akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Agosti 13,2019 amesema dereva huyo amefikishwa hospitali ya mkoa wa Ruvuma kwa matibabu zaidi kwani ana michubuko kidogo na amevunjika mbavu.

Amesema uchunguzi zaidi unaendeleaje kujua chanzo cha ajali hiyo ingawa  shehena ya mafuta lita 33,000 alizobeba zimekutwa salama na mmiliki wa mafuta hayo ameshahamisha kwa msaada wa ulinzi wa polisi na hajalalamika kuibiwa mafuta yake.

Endelea  kufuatilia Mwananchi kwa habari hii