Diamond : Natamani kufanya kazi na Usher Raymond

Muktasari:

Diamond alisema hayo katika mahojiano na tovuti ya Grammy iliyotaka kujua alikutanaje na wanamuziki nyota walioshinda tuzo kubwa nchini Marekani.

 

Dar es Salaam. Nyota wa muziki wa Bongo Fleva, Diamond Platnamuz ameeleza jinsi anavyopasua anga la muziki Marekani, huku akisema anatamani siku moja arekodi wimbo na mwimbaji na mtunzi maarufu duniani, Usher Raymond.

Diamond, ambaye sasa anamiliki studio ya kurekodi muziki ya Wasafi, vyombo vya habari, majengo na kampuni ya michezo ya kubahatisha, alisema hayo alipohojiwa na tovuti ya tuzo za muziki Marekani ya grammy.com.

Diamond pia ameeleza kuwa kama ikitokea siku moja atashinda tuzo Grammy, tuzo kubwa za muziki duniani, atatumia wiki nzima kusajili na baadaye kufanya onyesho la bure uwanjani kusherehekea na mashabiki wake.

Katika mahojiano hayo yaliyofanywa kwa njia ya mtandao wa Google, Diamond anaeleza jinsi alivyokutana na wanamuziki nyota wa taifa hilo la Marekani walioshinda tuzo za Grammy-- Alicia Keys na Ne-Yo-- na baadaye kurekodi nao baadhi ya nyimbo, akisema angependa kufanya kazi na Usher Raymond kutimiza ndoto yake ya muda mrefu.

Kuhusu kushirikishwa katika wimbo wa Alicia Keys, ambao amepewa sekunde 26, Diamond alimshukuru mtayarishaji wake wa muziki.

"Hiyo ilitokana na Swizz Beatz," alisema Diamond akimzungumzia mume wa Alicia Keys aliyemshirikisha katika wimbo wake wa "Wasted Energy".

"Amekuwa akiniunga mkono tangu zamani. Nilipokuja Loas Angelesmwaka huu (kabla ya mlipuko wa virusi vya corona) kutumbuiza, alinipigia simu na kuniambia niende studio. Nilipoenda studio, nilimkuta Alicia Keys akirekodi wimbo.

"Swizz alikuwa kama anasema 'lazima uchangamkie hii na kuingiza ubeti'. Nilistuka kwamba walipendelea niwepo katika wimbo. Alicia alikuwa akiandaa albamu yake, kw ahiyo nikasema, "sasa hizi? sehemu yangu ni wapi?"

Diamond alisema Alicia alimtaka aweke vionjo vya bongo fleva kwa asilimia 100.

"Kwa hiyo hivyo ndivyo ilivyokuwa. Ilikuwa ni wakati mzuri kwangu kwa sababu  ni kitu tofauti kufanya kazi na msanii ambaye umezoea kumuona katika TV au kusikiliza nyimbo zake, siwezi hata kuelezea, nashukuru."

Kuhusu kushirikiana na Ne-Yo katika kibao cha "Marry You", Diamond alisema hilo lilifanikiwa baada ya kukutana naye Afrika Kusini katika tuzo za MTV Africa.

"Aliulizwa alipokuwa anahojiwa ni msanii gani wa Afrika anamjua, na Ne-Yo alisema ananijua," alisema Diamond.

"Niliiambia menejimenti yangu kama Ne-Yo ananijua, hatuna budi kufanya kitu. Ne-Yo ni msanii ambaye nimekuwa namfuatilia tangu nikianza muziki. Baadaye meneja wangu aliniambia Ne-Yo anataka kuniona. Alipokuja Nairobi, mameneja wetu waliwasiliana. Nilikwenda Nairobi, na tukarekodi wimbo.

"Aliporejea Marekani, nilikwenda Los Angeles, tukapiga picha za video. Ndivyo colabo ilivyokuja. Sikumtegemea kuwa mchapakazi, kufanya wimbo wangu, na kuniunga mkono. Ni kama kaka kwangu.

Katika mahojiano hayo, Diamond pia alieleza mbinu alizotumia kuchomoza katika muziki, akisema aliona wasanii wengi hawatumii madansa hivyo akaanza kuwatumia na kujitofautisha na wengine.

Pia alisema wasanii wa bongo fleva hawakuwa wanatumia mabaunsa, lakini alipoanza tu kila mmoja alimuiga, huku yeye akiendelea kupata umaarufu.