Diamond Platnumz atoa majibu posti ya Alikiba

Dar es Salaam. Diamond Platnumz amezungumzia kilichoandikwa na msanii mwenzake, Ali Kiba katika mtandao wake wa  kijamii wa Instagram saa chache baada ya  kumualika kushiriki tamasha la Wasafi litakalofanyika Novemba 9, 2019.

Akizungumza jana Ijumaa Novemba Mosi, 2019 katika televisheni ya Wasafi nyota huyo wa kibao cha “Number One” amesema hakujua Ali Kiba alilenga nini, akibainisha kuwa hawezi kuwa na chuki naye.

Diamond alikuwa akizungumzia sintofahamu iliyoibuka Oktoba 30, 2019 kati yake na Ali Kiba.

Siku hiyo  aliulizwa swali katika mkutano wake na waandishi wa habari kama Ali Kiba na Harmonize watashiriki katika tamasha la Wasafi.

Alijibu kuwa ameuandikia uongozi wa Ali Kiba kuomba ushiriki wa mtunzi huyo wa wimbo maarufu wa “Aje”.

Pia Diamond, ambaye jina lake halisi ni Nassib Abdul, alisema hakuna haja ya kuendeleza “bifu (mzozo) ambao hakuutaja, baina yake na Ali Kiba.

Lakini kauli yake kwa waandishi wa habari haikumfurahisha Ali Kiba na katika akaunti ya mtandao wa kijamii ya officialalikiba, alitoa maneno makali bila ya kumtaja anayemshambulia.

“Usiniletee mambo ya darasa la pili, unaniibia penseli halafu unanisaidia kutafuta,” ameandika bosi huyo wa Kings Record Label.

“(UNIKOME). Mwanaume huwa anaongeaga mara moja tu, sasa ukitaka nikuweke uchi watu wajue unayonifanyia hata kwenye hilo tamasha hatokuja mtu. Sasa tuishie hapo, nakutakia tamasha jema.”

Juu ya ujumbe huo kuna picha ya Ali Kiba akiwa amekaa kwenye kiti, amevalia suruali aina ya jeans na shati la mikono mirefu bila ya kufunga vifungo.

Jana katika mahojiano hayo Diamond amesema, “nilibahatika kuona post kama watu wengine, na sikujua alilenga kitu gani,  lakini Alikiba ni kaka yangu amenizidi umri alianza muziki kabla yangu.”

“Kwenye muziki kuna mambo ya ukitoa wimbo ni kama Simba na Yanga (timu za soka zenye upinzani nchini Tanzania) lakini haiwezi kutia chuki kati yangu na yeye,” amesema Diamond.

Diamond ambaye wimbo wake wa “Number One” (remix) ulitamba Afrika baada ya kumshirikisha Davido wa Nigeria amesema, “japo sijajua sababu, mimi ni mtu ninayeheshimu sanaa naamini ni miongoni mwa watu tunaochangia kuleta sifa katika tasnia ya muziki nchini.”

Kuhusu tuzo za Afrimma zilizofanyika Marekani ambazo alikuwa miongoni mwa wasanii waliotakiwa kupanda jukwaani, Diamond amesema alishindwa kutumbuiza, akibainisha kuwa suala hilo linaihusu menejimenti yake.

Diamond pia alizungumzia kuhusu Harmonize ambaye ametangaza kujiondoa kampuni ya WCB, “Nimempush Harmonize kufika hapo alipo, nafikiri sasa ni wakati sahihi wengine kuwasapoti, tamanio letu ni kuona tunafanikiwa, naomba watu wamsapoti lengo letu ni kusapoti vijana.”