Diwani ACT- Wazalendo akata rufaa, kesi kusikilizwa Oktoba 29

Monday October 21 2019

 

By Happiness Tesha, Mwananchi [email protected]

Kigoma. Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, imeahirisha kesi ya Diwani wa Mwanga Kaskazini (ACT-Wazalendo), Manispaa ya Kigoma Ujiji, Clayton Chipando, maarufu Baba Levo, hadi Oktoba 29, 2019  baada ya Jaji mfawidhi wa mahakama hiyo Llvin Mgeta anayesikiliza kesi hiyo kupata dharura ya kikazi.

Akiahirisha kesi hiyo mahakamani hapo leo Jumatatu Oktoba 21, 2019 Jaji mfawidhi wa mahakama hiyo Athumani Matuma amesema hawezi kusikiliza kesi hiyo kwani yupo Jaji mwenzake anasikiliza tangu awali.

Amesema Jaji anayesikiliza kesi hiyo amepata safari ya ghafla ya kikazi ambapo yeye ameipanga tarehe nyingine kwaajili ya kusikilizwa ili Jaji husika akirudi aweze kuendelea na kesi yake.

Wakili wa upande wa utetezi, Thomas Msasa amesema mteja wake amekata rufaa kwa sababu mbili kwanza hakuridhishwa na adhabu iliyotolewa ya mwaka mmoja na siku mbili.

Amesema kwa mujibu wa sheria ilitakiwa iwe kifungo cha mwaka mmoja lakini yeye aliongezewa siku mbili na pia kwa kutiwa hatiani na kuendelea kusisitiza  kutokufanya kosa hilo.

Naye wakili wa upande wa serikali, Robart Magige ameiomba mahakama hiyo kupata mwenendo wa kesi hiyo kutoka mahakama ya mwanzo ili waweze kujibu rufaa hiyo wakati wa kesi kusikilizwa.

Advertisement

Diwani huyo amekata rufaa ikiwa ni mara ya pili ambapo mara ya kwanza mnamo  Agosti 8, 2019 alihukumiwa miezi mitano kwenda jela na kufikia  Agosti 2,2019 alikata rufaa kupinga hukumu hiyo.

Septemba 10, 2019 mahakama ya hakimu mkazi wilaya ilimuhukumu kifungo cha mwaka mmoja na siku mbili diwani huyo ambapo Oktoba 10, 2019 alikata rufaa tena.

Baba Levo ambaye pia ni msanii wa kizazi kipya anashtakiwa kwa kosa la shambulio la kudhuru mwili kwa askari wa usalama barabarani ambapo inadaiwa mnamo Julai 15, 2019 majira ya saa moja jioni maeneo ya kwa Bela alitenda kosa hilo.

Advertisement