Diwani aomba vipimo vya corona kwenye vivuko, Serikali ya Tanzania yamjibu

Muktasari:

Baraza la madiwani  Halmashauri ya Buchosa  wilayani Sengerema Mkoa wa Mwanza limeiomba Serikali  kuweka vipimo vya ugonjwa wa corona kwenye vivuko vinavyotoa huduma ya usafiri katika visiwa vya Kome na Maisome.

Buchosa. Baraza la madiwani  Halmashauri ya Buchosa  wilayani Sengerema Mkoa wa Mwanza limeiomba Serikali  kuweka vipimo vya ugonjwa wa corona kwenye vivuko vinavyotoa huduma ya usafiri katika visiwa vya Kome na Maisome.

Kauli hiyo imetolewa na diwani wa Nyakasasa,  Ivo Deogratias leo Jumanne Machi 31, 2020 kwenye kikao cha baraza hilo.

Amesema kivuko cha Mv Kome na Mv Tegemeo havina vifaa vya kupimia corona, kushauri Serikali kuzingatia jambo hilo.

Halmashauri ya Buchosa ina visiwa zaidi ya 14 ambavyo vina mwingiliano wa watu kutoka maeneo mbalimbali, wengi wakiwa ni wafanyabiashara wa samaki na hutumia vivuko hivyo.

 

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Buchosa, Crispin Luanda amesema wameshaagiza vifaa hivyo serikalini na vikiwasili  vitawekwa kwenye vivuko hivyo.

"Kuanzia leo na kuendelea vipimo hivyo vitawasili na vitawekwa kwenye  vivuko hivyo wataalamu wa afya wapo kwa ajili ya kufanya kazi hiyo,” amesema Luanda.

Hoja ya Deogratias iliungwa mkono na diwani wa Bulyaheke, Bageti Ngele aliyeongeza kuwa Serikali  ikifanya hivyo itakuwa imewasaidia wananchi.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Buchosa,  Joseph Kanyumi ameitaka serikali kuharakisha kununua vifaa hivyo kuwanusuru wananchi.