VIDEO: Dk Bashiru aipongeza kauli ya Lusinde kuhusu Kinana, Makamba na Nape

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ally

Muktasari:

  • Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ally amempongeza mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde aliyemuomba Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola kuagiza polisi kumhoji Nape Nnauye na Abdulrahman Kinana

Dodoma. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ally amempongeza mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde aliyemuomba Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola kuagiza polisi kumhoji Nape Nnauye na Abdulrahman Kinana.

Dk Bashiru ametoa kauli hiyo leo Jumanne Julai 23, 2019  mkoani Dodoma katika mkutano na wanachama wa chama hicho mkoani humo.

Jumamosi Julai 20, 2019 Lusinde, ambaye amepachikwa jina la “Kibajaj” alizungumza na waandishi wa habari kuhusu sauti zilizosambaa mitandaoni zikidaiwa kuwa ni za Nape, ambaye ni mbunge wa Mtama na Kinana, aliyekuwa katibu mkuu wa CCM, zikimtaja Rais John Magufuli katika masuala mbalimbali.

Mbunge huyo alitaka wawili hao kuhojiwa na polisi kuhusu sauti hizo, kuahidi atakaporejea katika safari yake ya China atazungumza kuhusu sauti zinazodaiwa kuwa za makada mbalimbali wa CCM.

Si Nape wala Kinana, ambaye hivi karibuni aliandika waraka kwa baraza la ushauri la viongozi wastaafu kulalamikia kuchafuliwa, aliyejitokeza kuzungumzia sauti hizo, wala hakuna waliothibitisha kuwa sauti hizo ni za makada hao, lakini Lusinde anataka wawili hao wahojiwe.

Katika maelezo yake ya leo, Dk Bashiru amesema Lusinde alifanya jambo jema kuhakikisha hali ya hewa iliyochafuka, inakuwa safi.

"Fanyeni kazi ya uenezi, nampongeza Lusinde alipoona hali ya uwanja si nzuri alifungua mlango wa chooni akapuliza pafyumu, akatokea  mlango wa nyuma akapaa zake China, safi sana," amesema Dk Bashiru.

Amewasifu viongozi wa CCM Mkoa wa Dodoma kwa kutoa tamko la kukemea barua inayoandikwa na Kinana na katibu mkuu mwingine wa zamani wa chama hicho, Yusuf Makamba kwenda kwa katibu wa baraza la ushauri la viongozi wakuu wastaafu wa chama hicho wakilalamika kudhalilishwa kwa mambo ya uongo na mtu aliyejitambulisha kuwa mwanaharakati na mtetezi wa Serikali.

Juzi Katibu mwenezi wa CCM Mkoa wa Dodoma,  Henry Msunga alisoma tamko la chama hicho wakilaani barua hiyo ya Kinana na Makamba na kutaka chama kiwashughulikie.