Dk Bashiru aitaka UDSM kupaza sauti Zimbabwe kuondolewa vikwazo

Muktasari:

Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) zimekubaliana Oktoba 25 ni siku ya kupaza sauti kwa mataifa ya Ulaya kuiondolea vikwazo Zimbabwe, siku hiyo pia ni kumbukumbu ya kuanzishwa UDSM. Hivyo uongozi wa chuo hicho umeombwa kuitumia siku hiyo kupaza sauti kitaaluma kushinikiza nchi ya Zimbabwe iondolewe vikwazo.

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ally ameutaka uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)  kuungana na nchi wanachama wa Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ( SADC) kupaza sauti Zimbabwe iondolewe vikwazo.

Dk Bashiriu amesema hayo jana Alhamisi Agosti 22,2019 alipokuwa anazindua mradi wa kuwasha taa za barabarani  zinazotumia nishati ya jua Mtaa wa Chifu Kunambi  chuoni hapo.

Alisema wakati wakisherehekea kumbukizi ya kuanzishwa kwa chuo hicho Oktoba 25, 2019 waendeshe pia matukio ya kitaaluma ya kuunga mkono juhudi za viongozi wa  SADC za kuhakikisha Zimbabwe inaondolewa vikwazo.

"Oktoba 25 mwaka huu ninajua ni kumbukumbu ya kuanzishwa kwa UDSM, tarehe hiyo pia imepangwa na wakuu wa SADC iwe ni siku ya kutoa tamko kwa mataifa ya Ulaya kuiondolea vikwazo Zimbabwe, niwaombe na nyie mshiriki katika mpango huo siyo kwa kupiga kelele bali kwa kuendesha matukio ya kitaaluma," alisema Dk Bashiru.

Alisema chuo hicho kina kumbukumbu nzuri ya ukombozi wa bara la Afrika, hivyo kuungana na mataifa mengine kuipambania Zimbabwe ni miongoni mwa mapambano hayo ya kitaaluma.

Kuhusu mradi wa taa Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa  William Anangisye alisema mradi huo ulioanza Juni na kukamilika Julai,  umegharimu kiasi cha dola za Marekani 49,300  sawa na  Sh113 milioni  na kumewekwa nguzo 36 zenye kifaa cha sola kila moja na zina uwezo wa kufanya kazi kwa saa 50,000 bila kubadilishwa.

Alisema taa hizo zimefungwa mfumo maalumu unaoziwezesha kujiwasha ikifika usiku na  kujizima ikifika asubuhi.

“Mradi huu ni wazo la Dk Bashiru ambapo aliuomba ubalozi wa china kufadhili ujenzi wa taa hizo baada ya kuwapo kwa changamoto kadhaa kwenye eneo hilo, ”alisema.

Alifafanua kuwa kuwapo kwa taa hizo kutaimarisha ulinzi na usalama katika mtaa huo, zitapunguza gharama za  malipo ya umeme na fedha zilizokuwa zikitumika kulipa Tanesco zitapangiwa matumizi mengineyo.

Naye Balozi wa China nchini Tanzania, Wang Ke alisema, "Tulipokea ombi la kujenga taa kutoka kwa Dk Bashiru Ally na Profesa Anangisye, nilipotembelea ni kweli nikaona kuna giza, nikaona kuna umuhimu wa kuweka taa kwani zinawekwa katika maeneo muhimu pia ni usalama.”

Alifafanua hawataacha kuisaidia Tanzania, kwani wamekuwa wakifanya hivyo mara nyingi na kwa miradi mbalimbali.