Dk Bashiru akana CCM kununua wabunge na madiwani

Dar es Salaam. Wakati wimbi la viongozi mbalimbali wa vyama vya upinzani wakiwemo wabunge na madiwani kuendelea kuhama vyama vyao na kujiunga na Chama cha Mapinduzi CCM, katibu mkuu wa chama hicho, Dk Bashiru Ally amesema hakuna mtu anayenunuliwa kujiunga CCM.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Machi 2, 2020 amesema idadi ya watu wanaohamia ndani ya chama hicho kutoka vyama vya upinzani ni kubwa kiasi ambacho huwezi kuwa na uwezo wa kuwanunua wote.

"Madiwani waliohamia CCM tangu 2016 wameshafikia 300, vyama vilivyozalisha hao madiwani Chadema inaongoza zaidi ya 200, mpaka ACT yenye madiwani wachache imekonda wanane wameondoka," Dk Bashiru.

Dk Bashiru amesema kuwa wabunge ambao wameshajiunga na chama hicho kutoka vyama pinzani ni majimbo 13 ambayo wabunge wake wote sasa wameondoka na majimbo hayo kunyakuliwa na CCM.

Kutokana na hilo amehoji kuwa unakuwa na uwezo gani wa kuwanunua watu zaidi ya 300, wabunge zaidi ya 13 na wanachama wanaojiunga na chama hicho.

Amewataja baadhi ya viongozi waliokuwa kamati  kuu za vyama vya upinzani kama Edward Lowasa aliyekuwa mgombea wa Chadema nafasi ya urais na mjumbe wa kamati kuu, Fredrick Sumaye aliyekuwa mjumbe wa kamati kuu Chadema, Dk Mashinji aliyekuwa Katibu Mkuu Chadema akihoji watu hao wamenunuliwa kwa shilingi ngapi?

Vilevile, Dk Bashiru amesema kuwa suala la kuhama vyama ni la kikatiba na ni la kawaida kwani hata CCM imeshapoteza wanachama wao waliojiunga na vyama vingine huku akimtolea mfano Lazaro Nyalandu ambaye sasa ni mwenyekiti wa Kanda ya Kati Chadema.

“Hatukuwahi kununua yeyote, hatuna mpango wa kununua yoyote, hatuna pesa ya kupoteza rushwa ni adui wa haki na hatuwezi kutenda rushwa, lakini kuvutia? mlango uko wazi, karibu nyumbani kumenoga” amemalizia Dk Bashiru