Dk Bashiru aonya wanaotumia jina lake, Rais Magufuli kusaka uongozi

Muktasari:

  • Katibu Mkuu wa chama tawala nchini Tanzania CCM, Dk Bashiru Ally ameanza ziara ya siku tatu mkoani Tanga yenye lengo la kuimarisha chama
  • Kuna baadhi ya wagombea wanakwenda kwa waganga wa kienyeji kutafuta uongozi,huo unakuwa ni uongozi wa laana kwani hauna baraka za wananchi na Mungu.

Handeni. Katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi,(CCM) Dk Bashiru Ally amesema yeye na mwenyekiti wa chama hicho, Rais John Magufuli hawana mgombea na wanasimamia masuala ya chama tu.

Dk Bashiru amesema hayo leo Jumatatu Januari 13, 2020  wilayani Handeni mkoani Tanga kwenye ziara yake ya siku nne mkoani humo.

Amesema wapo wagombea ambao wameanza kujitangaza kwamba wanaungwa mkono na katibu pamoja na mwenyekiti wake.

Amesema wameshaweka mtandao wao kufuatilia viongozi mbalimbali wa uongozi kufuatilia nyendo zao ili kubaini ni mambo gani wanafanya wakiwa kwenye majimbo.

"Wapo wengine nasikia wanatumia jina langu na la mwenyekiti wakijitamba wao ni majembe na sisi tunafahamu na kuwaunga mkono. Katibu mkuu na mwenyekiti hatuna mgombea," amesema Dk Bashiru.

Aidha Dk Bashiru ameonya tabia ya wagombea kutumia nyumba za ibada kwenda kuongelea mambo ya kisiasa na kusema kwamba utaratibu huo sio mzuri na haukubariki.

Amesema kama kiongozi amefanya vizuri aachwe hata kama ni miaka 100 ila kama amefanya vibaya hata kama ni mwaka mmoja aondolewe.