VIDEO: Dk Bashiru asema kama tatizo urais tukutane na Membe uwanjani

Muktasari:

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amemtaka aliyekuwa kada wa chama hicho, Bernard Membe kugombea urais kwa tiketi ya  chama kingine cha siasa ili wakutane uwanjani.

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amemtaka aliyekuwa kada wa chama hicho, Bernard Membe kugombea urais kwa tiketi ya  chama kingine cha siasa ili wakutane uwanjani.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Machi 2, 2020 alipotembelea ofisi za kampuni ya Mwananchi Communication Ltd (MCL) inayochapisha magazeti ya Mwananchi, Mwanaspoti na The Citizen baada ya kuulizwa kuhusu alichokisema Membe baada ya kuvuliwa uanachama.

Wiki iliyopita Membe alilieleza Mwananchi kuwa amevuliwa uanachama kutokana na nia yake ya kutaka kupambana na mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho katika uchaguzi mkuu wa 2020.

Katika maelezo yake leo, Dk Bashiru amesema katiba haisemi kama ukishafukuzwa kwenye chama hauruhusiwi kugombea kwenye chama kingine hivyo Membe aende na nguvu zake pamoja na wafuasi wake wakutane uwanjani.

“Ukishafukuzwa kwenye chama cha CCM katiba haisemi huwezi kugombea kwenye vyama 19 vilivyobaki, ila ukifungwa ndio unaweza ukakosa sifa au ukikwepa kodi, adhabu aliyopewa (Membe) haihusu sharia za nchi,” amesema Dk Bashiru.

Membe na makatibu wakuu wawili wastaafu,  Abdulrahman Kinana na Yusufu Makamba  walifikishwa mbele ya kamati ndogo ya udhibiti na nidhamu kujibu mashtaka ya kinidhamu.

Waliingia matatani baada ya sauti zao pamoja na za wanachama wengine watatu, kusambaa katika mitandao ya kijamii zikizungumzia kuporomoka kwa chama hicho na uenyekiti wa Magufuli.

Makamba amesamehewa makosa yake, Kinana atakuwa chini ya matazamio kwa miezi 18, kipindi ambacho hataruhusiwa kugombea uongozi, wakati Membe amevuliwa uanachama na hivyo hataweza kutimiza ndoto yake ndani ya chama hicho.

Kwa mujibu wa katiba ya CCM, nafasi ya kugombea urais iko wazi kwa mwanachama yeyote, lakini utamaduni wa chama hicho ni kumpa Rais aliyepo madarakani kuwania muhula wa pili, lakini Membe alitaka kuachana na utamaduni huo.