Dk Bashiru ashtuka, awaonya Wana CCM waache kuwageuza wabunge wao ATM

Muktasari:

Wanachama wa CCM wametakiwa kutowageuza wabunge wao vitega uchumi

Tabora. Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally, amewataka wanachama wa chama hicho kutowageuza wabunge kuwa vyanzo vyao vya mapato au sehemu ya kutolea pesa, ATM.

Akizungumza katika mkutano mkuu wa Jimbo la Nzega leo Jumapili Desemba 8, 2019, amesema wapo wanaowategemea wabunge kujipatia fedha.

“Muache kuwapigia simu wabunge kuwaomba pesa na vocha,” ameonya Bashiru.

Amewaambia wajumbe zaidi ya 400 kuwa kuomba ni kuvunja masharti ya CCM yanayomtaka mwanachama kufanya kazi, akisema kufanya kazi ndiyo kunawapa wana CCM heshima.

Amewananga baadhi ya wenyeviti wa chama hicho nchini, kushinda ofisini pasipo kufanya kazi na kugeuka kugombana na makatibu wao.

Amesema mwisho wa wenyeviti hao baada ya kugombana na makatibu wao ni kumpigia yeye simu wakiomba katibu ahamishwe.

Ameeleza kuwa wakati akiwa katika timu ya kufuatilia mali za chama iliyoundwa na Rais John Magufuli, alishuhudia mwenyekiti akigombana na katibu wake kuhusu fedha za kodi.

Amesema baadhi ya migogoro iliyopo ndani ya chama hicho inatokana na maslahi binafsi na kuongeza sasa fedha za kodi haziwezi kufujwa kutokana na udhibiti uliopo.

Awali, mbunge wa Nzega, Hussein Bashe alimweleza Dk Bashiru kuwa wanachama na wakazi wa Nzega watamuunga mkono Rais Magufuli, atakapogombea Urais mwakani.

Amesema katika kumuunga mkono, watachangishana fedha za kumchukulia fomu kwa kiasi chochote kitakachotakiwa kutokana na imani yao kwake na Chama cha Mapinduzi.