Dk Bashiru ataja mambo makuu manne yatakayoupaisha mkoa wa Dar es Salaam

Saturday October 05 2019
pic bashiru

Dar es Salaam.Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) cha nchini Tanzania, Dk Bashiru Ally amesema mkoa wa Dar es Salaam unafanya vizuri kimaendeleo kutokana na mambo makuu manne.

Amesema kama Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda atazidi kuyasimamia na kuyafanyia kazi vizuri na kuboreshwa, yataendelea kupaisha maendeleo ya jiji hilo.

Dk Bashiru ameyasema hayo leo Jumamosi Oktoba 5, 2019 katika Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam kulikofanyika mkutano wa CCM Mkoa wa kupokea utekelezaji wa Ilani ya chama hicho.

Katika Mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesoma utekelezaji wa Ilani mkoani humo.

Dk Bashiri amesema jambo la kwanza ni sekta ya kodi. Amesema Dar es Salaam inaongoza kuwa na idadi kubwa ya walipa kodi nchini, lakini ina changamoto kubwa ya wakwepa kodi sugu.

Amewataka wananchi kulipa kodi kwa hiari na wasimamizi wa kodi nao watende haki kwa kuweka mifumo mizuri ya uwazi na kushughulikia migogoro ya kodi katika mazingira ya uhusiano bora.

Advertisement

“Nimeliona kwenye ripoti yako nilisisitize na niwapongeze mnalifanya vizuri,” amesema Dk Bashiru.

Jambo la pili amezungumzia ulinzi na usalama, amesema kama Dar es Salaam haitakuwa salama, basi nchi nzima haitakuwa salama.

Amewataka mabalozi mkoani humo kushirikiana na uongozi wa mkoa, wilaya na vyombo vya usalama kuulinda mkoa wao.

“Baadhi ya Watanzania wanakejeli vyombo vyetu vya ulinzi na usalama, wanavichokonoa na kuvibeza na wakati mwingine wanavishambulia. Kweli vinaweza kuwa na dosari au changamoto ya utendaji ila wanafanya kazi nzuri,” amesema katibu mkuu huyo.

Amewapongeza Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola, Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Simon Sirro na Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa kwa kuhakikisha ulinzi wa jiji hilo unaimarika kila kukicha.

Eneo la tatu amelitaja kuwa ni utamaduni, michezo, sanaa na vyombo vya habari. Dk Bashiru amesema bila Dar es Salaam, Tanzania haiwezi kufanya vizuri kimataifa kwa sababu mchango mkubwa wa ukuaji wa maendeleo ya mkoa huo umechangiwa na vyombo vya habari.

“Vyombo vya habari vifanye kazi kwa kuwajibika, kukosoa kwa adabu na kwa misingi ya maadili pamoja na kujenga matumaini katika jamii kwamba kesho ni bora kuliko leo,” amesema Dk Bashiru.

 

Eneo la mwisho, amelitaja kuwa ni mazingira na kueleza kuwa jiji hilo ni uso wa nchi pindi wageni wanapokuja.

Amesema kama likichafuka kutokana na idadi ya watu, madhara yatakuwa makubwa kiafya.

“Nakupongeza Makonda kwa kampeni ya usafi. Nimeambiwa kuna viwanda vinavunja sheria na kuchafua mazingira na kuweka maisha ya watu mashakani kiafya. Naomba mshirikiane na taasisi zinazohusika tuhakikishe sheria inasimamiwa,” amesema Dk Bashiru.

Mbali na hayo, amewataka wakazi wa Dar es Salaam kujiandikisha katika daftari la mpiga kura, kazi inayoanza rasmi Oktoba 8 hadi 14  katika vituo 1,458 vilivyotengwa.

Amesema Wilaya ya Temeke itakuwa na vituo 474, Kigamboni 155, Ubungo 187, Ilala 379 na Kinondoni 265 kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 24, mwaka huu.

Advertisement