Dk Bashiru ataja siri ushindi wa CCM Serikali za mitaa

Muktasari:

Sababu za CCM kushinda uchaguzi wa Serikali za mitaa zimetajwa nyingi lakini moja ni wagombea wa chama hicho tawala nchini Tanzania kupewa bure fomu za kuomba ridhaa ya kuwania uongozi.

Unguja. Sababu za CCM kushinda uchaguzi wa Serikali za mitaa zimetajwa nyingi lakini moja ni wagombea wa chama hicho tawala nchini Tanzania kupewa bure fomu za kuomba ridhaa ya kuwania uongozi.

 

Hayo yameelezwa leo Jumamosi Novemba 30, 2019 na katibu mkuu wa chama hicho, Dk Bashiru Ally wakati akizungumza na wajumbe wa kamati za siasa Mkoa wa Mjini Unguja.

 

Amesema fomu hizo kugawiwa bure kiliwafanya wanachama wenye sifa na kukubalika kuchukua fomu kuomba kupitishwa kuwania uongozi.

 

Amebainisha kuwa utaratibu huo umeleta tija ikiwa ni pamoja na kuepusha baadhi ya watu kutumia fedha zao kuwalaghai wanachama.

 

Dk Bashiru amesema silaha nyingine ya ushindi huo ni moyo wa dhati wa kujitolea wa mawakala wa chama hicho aliodai kuwa hawakulipwa fedha yoyote.

 

 

Katika uchaguzi huo CCM ilizoa ushindi mitaa yote 4,263 nchini, vyama sita vya siasa vilipata  nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi huo uliofanyika Novemba 24, 2019.

 

Vyama sita kati ya 19 vilivyopata nafasi za uongozi ni CCM, Chadema, CUF, ACT Wazalendo, UDP na DP.

Hata hivyo, vyama vya Chadema, ACT Wazalendo na CUF vimetajwa kupata viti wakati vilitangaza kujitoa mapema.

 

Jumla ya wapiga kura milioni 19.6 walijitokeza kujiandikisha katika daftari la wapiga kura wa uchaguzi huo. Kati ya hao wanaume walikuwa ni milioni 9.5 na wanawake milioni 10.1.

 

Watu 539, 993 sawa na asilimia 97.3 walifanikiwa kurejesha fomu zao.

 

Vyama 19 vilivyoshiriki katika hatua mbalimbali za uchaguzi huo ni CCM, Chadema, CUF na ACT- Wazalendo.

 

Vingine ni NCCR-Mageuzi, UPDP, NLD, NRA, SAU, ADA, ADA-TADEA, TLP, UDP, Demokrasia Makini, DP, AFP, CCK, ADC, UMD na Chauma.

 

Katika orodha ya Waziri wa Tamisemi, Seleman Jafo vimo vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF, ACT-Wazalendo, UPDP na Chauma ambavyo vilitangaza kujitoa mapema.

 

Vyama hivyo vilijitoa vikilalamikia kukiukwa kwa mchakato mzima kutokana na wagombea wao kuenguliwa au kunyimwa fomu.

 

Nafasi ya uenyekiti wagombea wa CCM waliopita bila kupingwa walikuwa ni katika vijiji 12028, vitongoji 62,927 na mitaa 4207.

 

Katika  kundi la wanawake waliopita bila kupingwa walikuwa ni 105,953 wakati kwenye kundi la mchanganyiko walikuwa ni 131, 359.

 

Chadema kilipita bila kupingwa katika nafasi 69 ambapo kati ya hizo kundi la wanawake zilikuwa 27 wakati kundi la mchanganyiko 42.

Kwa upande wa CUF, kilipita bila kupingwa katika nafasi nane huku kundi la wanawake wakiwa watatu na mchanganyiko watano.

 

Kwa upande wa ACT Wazalendo waliopita bila kupingwa walikuwa 12, mmoja alipita katika kundi la wanawake na wagombea 11 kwenye kundi la mchanganyiko.