Dk Bashiru ataka ofisi za CCM kuwa maeneo ya kutoa haki

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ally

Muktasari:

Dk Bashiru amesema kwa kuwa CCM ndiyo  inayosimamia Serikali, watendaji wake hawana budi kushughulikia matatizo ya wananchi badala ya kusubiri viongozi wa juu.

Babati. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ally amesema hivi sasa ofisi za CCM zitakuwa nyumba za kutafutia haki.

Ameyasema hayo mjini Babati wakati akiweka jiwe la msingi la jengo jipya la ofisi za makao makuu ya CCM mkoa wa Manyara.

Amesema kutokana na chama hicho kusimamia Serikali, inapaswa ofisi zake ziwe nyumba za haki na kutoa haki za wananchi

"Kila mara Mwenyekiti wa CCM Rais John Magufuli anasimamishwa na wananchi na kuelezwa matatizo ambayo yanaweza kutatuliwa na mtendaji wa kijiji, ofisa tarafa au mkuu wa wilaya tunataka ofisi zetu ziwe nyumba za haki," amesema Dk Bashiru.

Kwa mujibu wa Katibu mwenezi wa CCM mkoa wa Manyara, Jacob Siay, ujenzi wa ofisi hiyo unakadiriwa  kutumia kiasi cha Sh650 milioni mpaka kukamilika kwake na hadi sasa zimetumika Sh368.9 milioni.

 

Siay amesema matarajio yao ni kumalizia ujenzi huo chini ya makadirio ya fedha zilizokusudiwa kutumika kwa ubora uliokusudiwa kwa mujibu wa maelekezo ya wataalamu wa ujenzi.

Naye mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Manyara Simon Lulu, amesema jengo hilo limechangiwa gharama zake na wanachama wa kawaida, ili kuondoa dhana kuwa limefikia hatua hiyo kwa kujengwa na wenye fedha.

"Wanachama wetu wamechangia fedha zao kidogo kidogo hadi kufikia hatua na siyo matajiri, hivyo kila mwanachama wa CCM Manyara anaweza kujivunia," amesema Lulu.