Dk Bashiru ataka wagombea CCM kutoa elimu ya kupiga kura

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ally

Muktasari:

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimelekeza wagombea wake kubadilisha upepo wa kampeni kwenye mikutano ya hadhara kwa kuwaelekeza wananchi jinsi ya kupiga kura katika siku zilizobaki

Mwanza. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ally amewaagiza wagombea na viongozi wa chama hicho kujielekeza kutoa elimu ya kipiga kura kwa wananchi kabla ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 28, 2020.

Pia, amewaonya watendaji wakuu wa chama hicho kwa ngazi ya mkoa na wilaya ambao maeneo yao yatashindwa kufanya vizuri katika Uchaguzi Mkuu wajiandae kufungasha vilago na kutafuta kazi nyingine.

Dk Bashiru ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Oktoba 16, 2020 wakati akizungumza na wanachama na wafuasi wa chama hicho katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

“Tumeshasema mambo mengi yaliyofanywa na yatakayofanywa kwenye ilani yetu, naelekeza kuanzia sasa tuanze kujielekeza zaidi kwenye elimu ya mpigakura na kuandaa mikakati ya ushindi,” amesema Bashiru.

“Niwaambie watendaji wote wa chama, kama eneo lako utashindwa jiandae kuondoka nafasi hiyo, atapewa mwingine na wewe unaweza kupangiwa kazi nyingine hata ukija kwenye ofisi yangu ukaanza kunipangia ratiba za kazi,” amesema