Dk Bashiru atua Pemba, atoa onyo uchaguzi mkuu 2020

Muktasari:

Katibu mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ally leo Jumatatu Desemba 2, 2019 amewasilia visiwani Pemba, Zanzibar kuanzia ziara ya siku tatu ya kukijenga chama huku akitoa onyo kwa wanachama kuelekea uchaguzi mkuu mwaka 2020.

Pemba. Chama tawala nchini Tanzania CCM, kimetoa onyo kali kwa  jumuiya za chama hicho na wanachama wake kisiwani Pemba, Zanzibar kutokubali kupoteza majimbo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kwani kufanya hivyo ni kuvunja katiba ya chama hicho.

Kimesema katiba yao inasema kila chaguzi ushindi kwao ni lazima.

Onyo hilo limetolewa leo Jumatatu Desemba 2, 2019 na Katibu mkuu wa chama hicho, Dk Bashiru Ally katika ziara yake Pemba akiwa wilaya ya Micheweni mkoa wa Kaskazini Pemba.

Amesema ushindi wa chama hicho utalindwa na jumuiya za chama hicho na ndiyo wenye jukumu kubwa.

“Sitakubali kusikia tumepoteza tena majimbo Pemba kwa kuwa kufanya hivyo ni kwenda kinyume na katiba yetu,” amesema

Amesema kila mwanachama afahamu kwamba ana wajibu wa kukilinda chama hicho pamoja na kulinda ushindi wake.

Pemba imekuwa ngome ya upinzani ambapo Chama cha Wananchi (CUF) kilikuwa kikishinda majimbo na wawakilishi huku CCM ikifanya hivyo Unguja.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi