VIDEO: Dk Bashiru awasha taa ya 2020

Dar es Salaam. Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally ametuma salamu kwa wagombea wa nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho tawala baada ya kufuta na kutangaza kurudiwa kwa uchaguzi wa wagombea uongozi wa serikali za mitaa maeneo mbalimbali yenye malalamiko nchini.

Dk Bashiru ametangaza kurudiwa kwa uchaguzi huo wa kura za maoni kwa wagombea wa chama hicho tawala katika maeneo yaliyolalamikiwa nchi nzima kwa kukiuka kanuni za uchaguzi huo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ndogo za makao makuu ya chama hicho Lumumba jijini Dar es Salaam juzi, Dk Bashiru pia aliutaja Mkoa wa Dar es Salaam kuwa una malalamiko mengi, hivyo akautaka urudie na kuhakiki mchakato wa uchaguzi.

CCM ilifanya uteuzi huo wa ndani ili kupata wagombea kwa ajili ya uchaguzi uliopangwa kufanyika Novemba 24.

Kitendo hicho cha kuchukua hatua za haraka na kuamuru uchaguzi huo kurudiwa maeneo yenye malalamiko kumetafsiriwa kuwa ni salamu kwa wagombea katika uchaguzi mkuu 2020.

Uchaguzi mkuu hushirikisha nafasi za udiwani, ubunge na rais.

Katibu wa NEC, siasa na uhusiano wa kimataifa wa CCM, Kanali Ngemela Lubinga amesema kitendo hicho kinatuma salamu kwa wote wenye tabia ya kutofuata utaratibu na waliozoea kutumia rushwa ili kupata uongozi.

“Katibu (Dk Bashiru) ameona kasoro na kutoa maelekezo. Unapoongoza mapigano unakuwa na operation order (amri ya mapigano), lakini mambo yanapobadilika huna budi kubadili mbinu,” alisema Lubinga na kuongeza kuwa “lazima chama kiwe makini kuhakikisha utaratibu uliowekwa, Watanzania wanauelewa.”

Alisema kuna faida kubwa kwa chama kutokana na ukweli kwamba sasa Watanzania ni waelewa, hawataki kudanganywa na kunapokuwa na waelewa zaidi wanaotaka kutumia hila za rushwa na udanganyifu ni lazima wazuiwe.

Hata hivyo, kauli hiyo inapingana na ile iliyotolewa na katibu mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji ambaye alihoji uadilifu wa jambo hilo.

“Ni lini CCM imebadilika? Huu ni ‘ukoo wa panya’, kila siku wanalalamika swali ni je, hao waliowafutia uchaguzi ni wakati gani walipewa nafasi ya kusikilizwa au ni muendelezo wa kuweka watu wanaowataka wao? alihoji Dk Mashinji.

Akizungumzia hilo, Profesa wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Mohamed Bakari alisema kwa hali ilivyo sasa iwe chama tawala au upinzani ni lazima vifuate taratibu ili kurahisisha kazi ya Uchaguzi Mkuu 2020.

“Hii ni kiashiria kwamba sasa umefika wakati wa chama tawala kihakikishe kinajisafisha kitaifa katika chaguzi zake zote ili ziwe huru na haki,” alisema.

“Wanapaswa kupita kwa ridhaa ya wananchi na siyo nguvu ya dola, ushindani uwe wa haki maana wananchi walishapoteza imani na kusababisha watu kususa kupiga kura kwa kuwa tu waliokuwa wana fedha ndiyo walioshinda chaguzi.

Suala la rushwa katika chaguzi halikuachwa bila kuzungumziwa.

Profesa Gaudence Mpangala alisema rushwa ilikuwa inatawala katika chaguzi mbalimbali.

“Ilifika mahali ilijulikana wazi kwamba bila kuwa na fedha kuanzia (Sh) milioni 50 au 100 huwezi kuwa mbunge, chama kilipoteza sifa kwa kiwango cha juu kwa sababu watu waliweka mbele rushwa,” alisema Profesa Mpangala.

“Ni lazima vyama vyote vijiandae katika hilo, ili kupata wagombea wenye sifa mwaka 2020 na si vinginevyo. Tusiishie kufuta bali wazunguke nchi nzima kutoa elimu ya uchaguzi badala ya hali ilivyo sasa, wapiga kura wanafikiri wakati wa uchaguzi ni kipindi cha kuvuna fedha,” alisisitiza mhadhiri huyo wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu).