Dk Bashiru azitaka taasisi za fedha kukopesha wakulima

Muktasari:

Katibu Mkuu wa chama tawala nchini Tanzania CCM ameendelea na ziara yake mkoani Kigoma ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya chama hicho kwa mwaka 2015/20.

Kigoma. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, Dk Bashiri Ally amezitaka taasisi za kifedha kuona uwezekano wa kuweka utaratibu mzuri wa kuwakopesha fedha wakulima wa zao la mchikichi mkoani Kigoma ili kuongeza tija kwa zao hilo ambalo ni zao la kimkakati.

Akizungumza leo Jumamosi Januari 18, 2020 mara baada ya kukagua kituo cha utafiti wa zao la mchikichi Kihinga kilichopo wilayani Kigoma ambapo amesema katika kuelekea katika uchumi wa viwanda sekta ya kilimo ni muhimu.

Amesema wananchi wakulima wakipata mitaji kilimo hicho kitaenda na kasi wanayoitaka wao huku wizara ya kilimo iweze kushirikiana na vyuo vya utafiti na vyuo vya kilimo nchini viweze kufufuliwa na kujipa jukumu la kufanya kazi ambazo Rais wa Tanzania, John Magufuli  angepewa kuona inafanyika.

"Tunatakiwa tutambue kilimo cha wakati huu ni cha kisasa tofauti na kilimo ambacho walikuwa wanalima zamani lazima tuongeze thamani katika kilimo chetu," amesema Dk Bashiru.

"Nimpongeze Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassimu Kajaliwa ambaye alikuwa anasukuma sana zao hilo lakini bado tuna safari ndefu, kama tukiwekeza katika kilimo cha mchikichi wakulima wetu watapata chanzo cha mapato ya fedha "amesema Dk Bashiru.