Dk Bashiru azungumzia majina yanayotumika kwenye matawi ya CCM

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally akifungua tawi la CCM la Ali Hassan Mwinyi katika Kata ya mzimuni Kawe jijini Dar es Salaam leo akiwa kwenye ziara. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Katibu Mkuu wa chama tawala nchini Tanzania cha (CCM) Dk Bashiru Ally leo Jumapili ameendelea na ziara yake katika majimbo ya Dar es Salaam kwa kufungua matawi ya chama hicho huku akionya matumizi ya majina kwenye matawi hayo

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa chama tawala nchini Tanzania cha (CCM) Dk Bashiru Ally amewataka wanachama wa chama hicho kuzingatia majina yenye ujumbe kwenye mashina wanayofungua badala ya kutaja majina ya wagombea.

Dk Bashiru ameyasema hayo leo Jumapili Septemba 1, 2019 wakati akizindua shina la ‘hapa kazi tu’ kata ya Kawe wakati wa ziara ya uimarishwaji wa chama hicho jijini Dar es Salaam nchini Tanzania.

Amesema majina yanayotakiwa ni yale yanayobeba ujumbe wa chama na Serikali na siyo majina ya wagombea katika nafasi mbalimbali.

"Tunataka majina yanayobeba ujumbe wa chama na Serikali na sio majina ya wagombea kwa kuwa chama hiki kina historia katika nchi hii," amesema Dk Bashiru

Amesema hakuna atakaye nyanyaswa na kero mbalimbali zinazowakabili zitashughulikiwa na Meya wa Kinondoni, Benjamin Sitta na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo  ambao ameambatana nao kwenye ziara hiyo watazishughulikia.

"Hakuna atakayenyanyaswa, mkiona mnasumbuliwa pigeni simu kwa mkuu wa wilaya, mkuu wa mkoa na wasipowasikiliza nipigieni mimi," amesema