Dk Kigwangalla: Mapato ya utalii Tanzania yameongezeka

Muktasari:

Wakati mapato yatokanayo na utalii nchini yakiongezeka katika mwaka 2018 hadi kufikia dola 2.4 bilioni za kimarekani (Sh5.4 trilioni) kutoka dola 2.2 bilioni za kimarekani (sawa na Sh5 trilioni) mwaka 2017 bodi ya utalii imeshauriwa kuongeza nguvu zaidi katika kutangaza utalii

 

Dar es Salaam. Mapato yatokanayo na utalii nchini Tanzania yaliongezeka mwaka 2018 hadi kufikia dola 2.4 bilioni za kimarekani (Sh5.4 trilioni) kutoka dola 2.2 bilioni za kimarekani (Sh5 trilioni) mwaka 2017.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa Oktoba 18, 2019 katika uzinduzi wa maonyesho ya utalii ya siku tatu nchini yaliyopewa jina la Swahili International Tourism Expo (SITE) yaliyoanza leo Oktoba 18 hadi 20, 2019 huku yakihusisha washiriki kutoka nchi 60 duniani kote.

Akizungumza katika ufunguzi huo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Khamis Kigwangallah amesema kadri nchi inavyozidi kujitangaza kimataifa imekuwa ni chachu ya ongezeko la watalii.

“Mwaka 2017 tulipata watalii milioni 1.3 na mwaka 2018 tulipata watalii 1.5 kati ya watalii milioni 67 waliotembelea vivutio mbalimbali duniani huku idadi yetu ya ikiongezeka ikiwa ni mara mbili ya ongezeko la watalii duniani,” amesema Dk Kigwangallah

Lakini wakati tamasha hilo likifanyika kwa mwaka wa tano mfululizo umaarufu wake umezidi kuongezeka huku likitengeneza fursa kwa wajasiriamali wadogo kuuza bidhaa zao.

Kwa upande wake, Katibu mkuu Kiongozi nchini Tanzania, Balozi John Kijazi aliyefungua maonyesho hayo aliitaka bodi ya utalii kuendelea kuboresha maonyesho hayo na mengine yanayotangaza utalii wa ndani na tamaduni za Tanzania ili kuongeza mapato kwa nchi.

“Kuna tamasha la urithi ambalo linafanya vizuri sana hivi sasa lifanyiwe maboresho zaidi lipate sura ya kimataifa ili lisaidie katika kuongeza mapato ya utalii,” amesema Kijazi