Dk Kijaji aonya utendaji kazi wa Tira

Muktasari:

Serikali ya Tanzania imesema kuwa hairidhishwi na mchango unaotolewa na mamlaka ya usimamizi wa shughuli za Bima (TIRA) kwenye mchango wa pato la Taifa ambao ni asilimia 0.53 kwa miaka kumi mfululizo na kuitaka iondoke hapo.

Dodoma. Naibu Waziri wa Fedha na Mipango nchini Tanzania, Dk Ashatu Kijaji  ameitaka mamlaka ya usimamizi wa shughuli za Bima (Tira) kuongeza juhudi kwenye utendaji wao wa kazi ili kuondokana na kiwango kidogo cha asilimia 0.53 inayochangia kwenye pato la Taifa.

Dk Kijaji ametoa kauli hiyo leo Februari 13, 2020 wakati akifungua mkutano wa baraza la wafanyakazi wa mamlaka hiyo Jijini Dodoma yenye lengo la kupitia bajeti ya mwaka 2019/20 na kutoa mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2020/21.

Amesema ni aibu kwa mamlaka kubwa kama hiyo kuchangia asilimia 0.53 kwenye pato la taifa kwa miaka kumi mfululizo hali inayoonyesha hawana ubunifu katika utendaji wao wa kazi na kuwataka wajitathimini upya.

“Lakini hapa nimekusikia mwenyekiti wa baraza hili kuwa mna mpango wa kuongeza mchango wenu kwenye pato la Taifa hadi kufikia asilimia tatu, hii nayo haitoshi hata kidogo haiwezekani mamlaka kubwa kama hii ichangie asilimia tatu tu kwenye pato la Taifa,” amesema Dk Kijaji na kuongeza kuwa;

“Nataka kikao hiki kitoke na suluhu la kuongeza mapato yenu ili machango wenu uonekane kwenye pato la Taifa na si hivi mnavyofanya sasa mnatakiwa kuionyesha serikali umuhimu wenu wa kuwepo hapo kwa kuongeza mchango wenu kwenye pato la Taifa.”

Aidha, ameitaka mamlaka hiyo kuongeza juhudi kwenye utoaji wa elimu kuhusu masuala ya bima ili Watanzania wengi waweze kujiunga hasa katika kipindi hiki ambacho serikali imedhamiria kuingia kwenye uchumi wa kati unaotegemea viwanda.

Amesema japo mamlaka hiyo ipo lakini wakulima wengi, wafugaji, wavuvi na wachimbaji wadogo wa madini nchini hawana bima zinazowalinda kwenye shughuli zao na kusababisha azma ya serikali kuingia kwenye uchumi wa kati kuwa na vikwazo vingi.

Mwenyekiti wa baraza hilo, ambaye pia ni Kamishna wa Bima nchini, Dk Mussa Juma amesema kuwa mpaka sasa wamewafikia asilimia 15 ya watu wazima kwenye huduma za bima na kusema kuwa lengo lao ni kuwafikia angalau asilimia 30 ya Watanzania wawe na bima hata moja

Amesema hiyo itawezekana kama wadau wote na wafanyakazi wa TIRA watashirikiana katika kufanikisha hilo kwa kuwa serikali inawategemea katika kufikia malengo hayo.