Dk Mahanga azikwa, Mbowe asifu unyenyekevu wake

Thursday March 26 2020
pic mahanga

Dar es Salaam. Mwili wa Dk Makongoro Mahanga ambaye alikuwa kada wa Chadema umezikwa makaburi ya Segerea wilayani Ilala huku mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe akisema enzi za uhai kiongozi huyo alikuwa nyenyekevu na muungwana asiyelewa madaraka.


Dk Mahanga aliyefariki dunia Machi 23, 2020 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu akisumbuliwa na ugonjwa wa pneumonia na mwili wake umezikwa katika makaburi hayo na mamia ya wananchi mbalimbali.


Katika salamu zake za pole zilizosomwa na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika kwa waombelezaji na familia Mbowe amesema pamoja na Dk Mahanga kukaa ndani ya chama kwa miaka minne na miezi tisa lakini aliweza kujipambanua.


"Mnyenyekevu lakini asiyeyumba kimsimamo hata fimbo za maisha, watawala na dola zilipobana. Alisimamia alichokiamini bila kujali athari za misimamo hiyo kwenye maslahi yake binafsi au famili yake," amesema Mbowe.

Katika salamu hizo Mbowe amesema "binafsi nasikitika sitaweza kushiriki kimwili kwenye maziko ya rafiki yangu na mpiganaji mwenzangu. Niko kwenye karantini ya wiki mbili ambapo siwezi kukutana na mtu yeyote hadi itakapothibitika kuwa nami siyo mwathirika.
"Hii ni kwa sababu mwanangu Dudley ni mojawapo wa wahanga wa kwanza wa janga la corona katika nchi yetu. Watalaamu wameishauri familia nasi tumeafiki kwa moyo mkunjufu umuhimu wa kufanya self isolation hadi itakapothibitisha kuwa hatunajambukizwa au hatuwezi kuambukiza wengine," amesema Mbowe katika salamu hizo.


Kwa mujibu wa Mbowe, safari ya kiasiasa na Dk Mahanga ilianza mwaka 2000 walipokutana bungeni kwa mara kwanza wakati huo Chadema ikiwa na wabunge watano akiwa mmoja wa viti maalumu.


Amefafanua kuwa katika ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa, Dk Mahanga aliketi safu ya viti nyuma akiwa karibu na jirani na rafiki yake Agrey Mwanri na ambaye walikuwa wakiitana 'home boy' kwa sababu walitoka halmashauri moja ya Hai mkoani Kilimanjaro.

Advertisement


Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Hamphrey Polepole alitoa pole kwa wanafamilia, jamaa na marafiki wa Dk Mahanga kwa msiba wa kiongozi huyo wa zamani akiwataka waendelee kumuombea kwa Mungu.
"Alikuwa CCM kisha kuhamia Chadema, lakini tuliendelea kumfahamu Dk Mahanga na msiba huu umetuleta pamoja watu wote. Mama (mke wa Dk Mahanga), simama imara Mungu yupo nanyi," amesema Polepole.


Ojambi Masaburi akisoma wasifu wa marehemu,  alisema Dk Mahanga alizaliwa Machi 4, 1955 katika kijiji cha Mugeta  wilayani Bunda mkoani Mara, kati ya mwaka 1965 hadi 1971 alipata elimu ya msingi katika shule za Ikizu, Mugumu na Kiambai.


"Mwaka 1972 hadi 75 alipata elimu ya sekondari ya Mara na mwaka 1976 hadi 78 alisoma kidato cha sita katika shule ya sekondari ya Tambaza. Shahada ya kwanza alipata mwaka 1983 na ya pili mwaka 1988 na mwaka 2000 alitunukiwa PHD," amesema.


Ojambi amesema enzi za uhai wake Dk Mahanga aliwahi kufanya kazi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) akiwa mkurugenzi wa  fedha na utawala na mhadhiri mwandamizi wa taasisi ya maendeleo ya jamii na mafunzo ya Nyegezi.

Advertisement