Dk Mashinji; Nilitamani kuendelea kuongoza Chadema

Dk Vincent Mashinji,

Muktasari:

Desemba 20, 2019 baraza kuu la Chadema lilimuidhinisha John Mnyika kuwa katibu mkuu wa akichukua nafasi ya Dk Vicent Mashinji aliyeshika wadhifa huo kwa miaka mitatu baada kuanzia mwaka 2015.

Dar es Salaam. Aliyekuwa katibu mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji amesema endapo angesalia kwenye nafasi ya ukatibu mkuu alipanga kuanzisha mapema mchakato wa kuwapata wagombea wa uchaguzi mkuu mwakani.

Amesema hayo jana Jumapili, Desemba 22, 2019 alipozungumza na Mwananchi zikiwa ni siku mbili tangu mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alipomteua John Mnyika kuchukua nafasi ya Dk Mashinji.

Alipoulizwa  kama bado alitamani kuendelea na ukatibu mkuu, Dk Mashinji alisema;  “`Yeah of course’ (ndio kwa kweli)” na hakutaka kueleza kwa undani kuhusu kutoteuliwa kuendelea na wadhifa huo.

Kuhusu jambo kubwa ambalo angelifanya iwapo angeendelea na cheo hicho amesema alitaka kuandaa mikakati ya chama hicho kushinda uchaguzi wa mwaka 2020.

“Kuhakikisha tunapata wagombea wanaotokana na wananchi, tungekwenda kutekeleza agizo la kamati kuu la kuwaomba wanaotaka kugombea urais, ubunge na udiwani wajitokeze. Wangetangazwa mapema ili wananchi waanze kuwatafiti hatimaye kumpata kiongozi anayetokana nao. Hilo lingefanyika kuanzia Januari mwakani,” amesema.

Mkakati huo amesema utasaidia kukijenga chama kwani kingewapa nafasi ya kujitambulisha kwa wananchi nao wangekishauri kuwapata wagombea wanaokubalika kwao. Wazo hilo pia liligusiwa na Mnyika jana (Jumapili) alipozungumza na waandishi wa habari alipokuwa akibainisha vipaumbele vyake vitano.

Dk Mashinji alidumu katika wadhifa huo kwa miaka mitatu tangu 2016 ameshauri nguvu kubwa ielekezwe kwa mgombea urais kwani ni muhimu wagombea wakajulikana mapema kwa wananchi ili wafahamike na wananchi wajue anayekuja kuwaletea mabadiliko wanayoyasubiri ni mtu wa aina gani.

“Katika nchi nyingine, wagombea urais wanajulikana hata mwaka mmoja au miwili kabla na hili linawafanya watu wachambue makandokando yake. Hata tukija kufanya kura ya maoni tunafanya kwa mtu anayejulikana,” amesema daktari huyo wa magonjwa ya binadamu na kusema iwapo Mnyika ataona inafaa anaweza kulifanyia kazi hilo.

Tangu alipoondolewa kwenye nafasi hiyo, Dk Mashinji amekuwa akiandika ujumbe wenye utata kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii na alipoulizwa kuhusu hilo amesema “kazi ya siasa ni kuwafikirisha watu, kuna wengine watasema hiki, mwingine atasema vile.”

Baadhi ya kauli zake aliyoiandika Twitter NI: “Haikuwa rahisi lakini tumetoka wote salama na tukiwa wamoja. Kichwani mwa kila kiongozi kumejaa siri nyingi sana... Eeh, Mungu mwenye enzi, nakushukuru sana kwa kutulinda mpaka tukatoka salama. Asanteni wana Chadema wote, na Watanzania kwa ushirikiano mwema!”