Dk Mashinji awaonya vijana Chadema, ataka kutoshambuliana

Muktasari:

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji amewataka vijana wa chama hicho  kutotumia muda mwingi kupambana wenyewe kwa wenyewe kwa maelezo kuwa mapambano ya chama hicho kushika Dola.

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji amewataka vijana wa chama hicho  kutotumia muda mwingi kupambana wenyewe kwa wenyewe kwa maelezo kuwa mapambano ya chama hicho kushika Dola.

Dk Mashinji ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Desemba 9, 2019 wakati akifungua mkutano mkuu wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) unaofanyika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Katika mkutano huo wa kuchagua viongozi wa baraza hilo, Dk Mashinji amesema katika mchakato huo wa uchaguzi kuna baadhi ya vijana majina yao yamekatwa kwa sababu mbalimbali ikiwamo kutokidhi vigezo hasa suala la umri, kuwataka kuwa kitu kimoja.

"Wale msiowataka na mnaowataka wote watumie kwa sababu wote ni wenu. Kila mmoja awatumie kwa wakati wake.”

"Vijana tambueni mapambano ya Chadema ni kushika dola ili kuifanya nchi kuwa na uchumi wa soko, demokrasia na haki. Mkibishana na mwenzako, bishaneni kuhusu madini, msigeuze mabishano kuwa sehemu ya ugomvi kati yenu," amesema Dk Mashinji.

Amesisitiza, “hivi  kwa nini mnabishana utadhani leo mtakufa? Mimi umri wangu ni miaka 47 kesho kutwa kuna uchaguzi unafanyika, naweza nisichaguliwe tena, lakini baadaye si naweza kugombea tena hata uwenyekiti. Sasa wewe una miaka 28 jina lako halipo Bavicha unaanza kulalamika.”

Amesema angependa kuona miaka ijayo vijana wa Bavicha wakawa viongozi wakubwa kama mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe aliyedai kuw alithubutu kutaka uongozi.

Amesema kipimo cha chama kukomaa ni kuibua mvutano lakini wanachama wakiingia ukumbini wanakuwa kitu kimoja na kusubiri sanduku la kura kwa ajili ya kufanya uamuzi.