VIDEO: Dk Mashinji awasili mahakamani, Halima Mdee akataa kumsalimia

Muktasari:

  • Aliyekuwa katibu mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji ambaye wiki iliyopita alihamia CCM leo asubuhi Jumatatu Februari 24, 2020 amefika katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kusikiliza kesi inayomkabili.

Dar es Salaam. Aliyekuwa katibu mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji ambaye wiki iliyopita alihamia CCM leo asubuhi Jumatatu Februari 24, 2020 amefika katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kusikiliza kesi inayomkabili.

Ilizoeleka kumuona Dk Mashinji akifika mahakamani kusikiliza kesi hiyo pamoja na  viongozi wanane wa Chadema, wote wakitokea chama kimoja lakini leo ni tofauti kwa kuwa sasa yupo CCM.

Dk Mashinji aliyevaa  shati la drafti na suruali nyeusi, baada ya kufika mahakamani alisalimiana na washtakiwa wenzake kwa kupeana mikono lakini alipofika kwa mbunge wa Kawe, Halima Mdee ambaye alikuwa akifuatilia jambo katika simu yake ya mkononi hakumpa mkono katibu mkuu huyo wa zamani wa Chadema.

Viongozi nane wa Chadema pamoja na Dk Mashinji wanakabiliwa na kesi ya uchochezi katika Mahakama hiyo, wanatarajiwa  kurusha karata yao ya mwisho kujaribu kujinusuru na hatia katika kesi hiyo.

Hii ni nafasi ya mwisho kwa wanasiasa hao kujinusuru, kwani watawasilisha hoja za mwisho mahakamani baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi na washtakiwa pia kumaliza kujitetea.

 

Dk Mashinji, viongozi wa Chadema wakiwemo mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe na katibu mkuu, John Mnyika, wanakabiliwa na mashtaka 13 yakiwamo ya kula njama, kufanya mikusanyiko na maandamano yasiyo halali na ya uchochezi wa uasi.

 Mbali ya Mbowe na Mnyika, wengine ni naibu katibu mkuu Salum Mwalimu (Zanzibar) na mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa.

Pia wamo mbunge wa Tarime mjini, Esther Matiko; mbunge wa Kawe, Halima Mdee; mbunge wa Bunda, Esther Bulaya; mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche.

Kwa pamoja wanadaiwa kutenda makosa hayo Februari 16, 2018 katika viwanja vya Buibui, wilayani Kinondoni wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Kinondoni.

Kesi hiyo inayosikilizwa na hakimu mkazi mkuu, Thomas Simba inaendelea leo katika hatua ya majumuisho ya hoja kutoka kwa mawakili wa upande wa mashtaka na utetezi, ili kuionesha mahakama iwapo washtakiwa wana hatia au la.

Hivyo kunatarajiwa kuwapo mchuano mkali wa kisheria kati ya mawakili wa pande hizo, kwani kila upande utakuwa na kibarua cha kuishawishi mahakama itoe hukumu ambayo itaunufaisha.

Washtakiwa kupitia jopo la mawakili wake linaloongozwa na Peter Kibatala watakuwa na kibarua cha kuishawishi mahakama kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yao, hivyo hawana hatia. Mawakili hao watalazimika kuchambua na kuonesha udhaifu wa ushahidi wa upande wa mashtaka.

Nao mawakili wa Serikali wakiongozwa na wakili mkuu wa Serikali, Faraja Nchimbi watakuwa na kibarua cha kupangua hoja za mawakili wa utetezi na kuishahawishi mahakama kuwa wamethibitisha mashtaka, hivyo washtakiwa wanastahili kutiwa hatiani kama walivyoshitakiwa.

Baada ya mchuano wa kisheria, hatima ya wanasiasa hao itabaki mikononi mwa mahakama itakapotoa hukumu kwa tarehe itakayoipanga.