Dk Mwinyi aahidi kuboresha masilahi ya walimu

Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk Hussein Mwinyi

Muktasari:

Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk Hussein Mwinyi amesema haiwezekani mwalimu anafundisha zaidi ya  miaka kumi bila kupanda daraja

 

Unguja. Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk Hussein Mwinyi, amesema iwapo atapata ridhaa ya kuongoza nchi, ataboresha masilahi ya walimu.

Dk Mwinyi ametoa ahadi hiyo  alipokuwa akizungumza na  walimu wa shule za msingi na sekondari ikiwa ni mwendelezo wa kampeni zake za kukutana na makundi mbalimbali na kusikiliza kero zao.

Amesema suala la rasilimali watu watalitizama kwa upana wake kwa kuangalia idadi ya walimu waliopo na taaluma zao na kusimamia mgawanyo wa walimu wa hisabati, sayansi na Tehama.

Dk Mwinyi amesema katika suala la vifaa vya kufundishia nako watalitizama vizuri kwa kuhakikisha vinawafikia wahusika.

Awali baadhi ya walimu waliomba akiingia madarakani aunde sheria ya kuwalinda na hatia mbalimbali.

Dk Mwinyi amelifafanua hilo kwa kusema: “Haiwezi kuundwa sheria ya kuwalinda kwa makosa ya jinai bali watalindwa kitaaluma, lazima tuwe wawazi katika hili ndani ya jamii kumeingia tatizo kubwa la udhalilishaji tupige vita kwa nguvu zote.”

 Amewaomba walimu kuwa miongoni mwa watakaoshiriki katika mapambano ya kupiga vita suala la udhalilishaji.

 “Inawezekana tatizo ni fedha au watendaji, pia suala la waimu kupanda madaraja nalo inabidi liangaliwe, haiwezekani una miaka zaidi ya 10 kazini anakuja kijana kuanza kazi mnakuwa sawa sawa,”amesema Dk Mwinyi.

Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu,  Mussa Omari Tafurwa amesema  sera ya elimu inapaswa kupitiwa upya kwa sababu mapitio ya mwisho yalifanyika mwaka 2006.

Mwalimu Sheikha Ali Khamisi amesema walimu wana hali ngumu inafikia mahali wanakata tamaa kwa kukosa nauli ya kwenda na kurudi shuleni.