Breaking News

Dk Mwinyi aahidi mazingira mazuri kwa Watanzania nje ya nchi

Sunday October 18 2020

 

By Kalunde Jamal, Mwananchi

Unguja. Mgombea urais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amewaita Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi kuja kuwekeza nchini, huku akiahidi Serikali kuwawekea mazingira mazuri ya uwekezaji.

Dk  Mwinyi ameyasema hayo leo Oktoba 18, katika ukumbi wa Hytt Park alipokuwa akizungumza na Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi.

Amesema  akiwa katika kampeni zake ameona akutane nao kwa sababu ni miongoni watu muhimu katika kujenga uchumi wa Zanzibar.

Amesema dhamira yake iwapo atapata ridhaa ya kuongoza nchi ni kufanya mapinduzi ya uchumi wa Zanzibar ambao unahitaji mambo kadhaa na viongozi wa juu wawe tayari kuyafanya.

"Kama nitakuwa rais, nitakuwa kiongozi namba moja na nipo tayari kuyafanya, jambo lingine ni watendaji lazima tuwe na nguvu ya watu wa kuwawezesha ili hayo mambo yatimie,” alisema.

Alisema ili kuinua uchumi wa nchi watatumia kila ambaye anaweza kusaidia wakiwamo waliopo ndani na nje ya nchi wakiwa Wazanzibari na wasio raia wa visiwa hivyo.

Advertisement

"Ili kuhakikisha lengo linatimia ndiyo maana nimeona tunahitaji kundi hili la diaspora liwe sehemu ya hao," amesema.

Dk Mwinyi amesema kuna maeneo kadhaa ambayo yanahitaji uwepo wao katika kukuza uchumi hasa wataalamu ambao wako tayari  kurudi kufanya kazi Zanzibar.

"Ahadi yangu nitamtumia kila mmoja, natambua wengine mmejenga maisha yenu nje sio rahisi kurudi, tunahitaji muwekeze hapa Zanzibar,  nyinyi wenyewe au kuleta wawekezaji kwa kuzungumza nao kule mlipo," amesema.

"Ahadi ya Serikali ni kulinda maslahi yenu kwa mlichowekeza na madai yenu ya kupata haki kama wazawa japo mpo nje ya nchi," amesema.

Amesema kuna kambi mbalimbali za afya zinafanywa nchini na diaspora ni nzuri, ila mtazamo wake wafikirie makubwa zaidi.

"Tufikiri makubwa zaidi, badala ya hizi kambi ndogondogo  tunataka huduma za kibingwa zifanyike hapa Zanzibar, leo tukipata mgonjwa wa moyo, upandikizaji wa figo, matibabu ya kubadili damu wanakwenda nje ya Zanzibar, tunataka wataalamu waje hapa.

" Kama ambavyo wenzetu pale Dar es Salaam, katika Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), kwamba magonjwa yote ya moyo yatibiwe hapa nchini, yale yanayoonekana makubwa yote yapatiwe tiba hapa badala ya kulazimika kupeleka magonjwa nje ya nchi," amesema.

Amewaeleza diaspora fursa zilizopo katika uchumi wa bahari kuwa upo katika maeneo manne ya utalii. "Hatujafanya utalii bado, tunafanya wa fukwe pekee, visiwa vyetu vina fursa ya kutosha kinachohitajika ni uwekezaji,” alisema.

Eneo lingine ni uvuvi akisema hakuna  kiwanda kikubwa cha samaki na haufanyiki uvuvi wa bahari kuu wala hakuna meli kubwa za uvuvi.

Amezungumzia pia eneo la mafuta na gesi kuwa ni fursa nyingine ya uwekezaji baada ya kugundulika kuwapo nyingi.

"Eneo la viwanda pia, kuna kundi kubwa la vijana hawana kazi tunahitaji kuwa na viwanda vya kusindika malighafi za bahari kama mwani, samaki na viwanda vingine vya nguo na kadhalika hizi zote ni fursa za uwekezaji. Kwa kifupi nataka muwe sehemu ya kuujenga uchumi mpya wa Zanzibar," amesema.

Wakizungumza katika mikutano huo baadhi ya diaspora walieleza kufurahishwa na nafasi ya kuzungumza na mgombea na kumweleza changamoto zao.

Ali Mbamba anayeishi Denmark amemshauri Dk Mwinyi iwapo atachaguliwa kuwa aikuze idara ya diaspora kwa kufanya wizara kamili.

Naye Abrahmani Rashid amesema  masuala ya kupata mikopo katika benki za nchini kwa diaspora ni changamoto  hususani kwa wawekezaji, hivyo akashauri idara iendelee kutoa elimu kwa wizara na taasisi za Serikali kuwatambua diaspora katika suala ya ajira.

Advertisement