Dk Omary Nundu afariki dunia

Wednesday September 11 2019

 

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Bodi ya kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania, Dk Omary Nundu (71) amefariki dunia.

Taarifa iliyotolewa leo mchana Jumatano Septemba 11, 2019 na Kitengo cha Mawasiliano cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) Dar es Salaam kimesema, “Waziri wa zamani Omary Nundu alifikishwa leo MNH, akitokea nyumbani kwa gari binafsi la wagonjwa akiwa tayari ameshafariki.”

“Hivyo waliomleta waliamua wakahifadhi mwili wake katika hospitali ya rufaa ya Jeshi Lugalo,” imeeleza taarifa hiyo

Dk Nundu enzi za uhai wake aliwahi kuwa mbunge wa Tanga na Waziri wa Uchukuzi katika Serikali ya awamu ya nne  ya Tanzania.

Juni 12, 2019, Rais wa Tanzania, John Magufuli alimteua Dk Nundu kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Airtel Tanzania ikiwa ni utekelezaji wa makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni ya Bharti Airtel International.

Katika makubaliano hayo, Mwenyekiti wa Bodi ya Airtel Tanzania pamoja na ofisa mkuu wa ufundi wanapaswa kuteuliwa na Serikali.

Advertisement

Kabla ya Dk Nundu aliyezaliwa Agosti 6 mwaka 1948 kuteuliwa alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL).

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi

Advertisement