Dk Stergomena: Nchi tatu zinasuasua kuridhia soko la pamoja Sadc

Wednesday March 18 2020

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasalimia

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasalimia washiriki wa Mkutano  wa Baraza la Mawaziri  wa Jumuiya  ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) alioufungua  kwa njia ya video kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam, Machi 18, 2020. 

By Kelvin Matandiko, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Jumuiya Maendeleo ya kusini mwa Afrika (Sadc), Dk Stergomena Tax amesema nchi tatu za jumuiya hiyo bado hazijaridhia makubaliano ya soko la pamoja hatua inayochelewesha mpango wa kikanda na Afrika. 

Dk Stergomena ametoa kauli hiyo leo Jumatano Machi 18, 2020 jijini Dar es Salaam nchini Tanzania wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Nchi 16 za jumuiya hiyo, akisema kwa sasa sekretarieti hiyo inaendelea na ushawishi wa nchi tatu zilizobakia kuwa sehemu ya itifaki ya soko la pamoja.

Mwaka 2019, waziri wa mambo ya nje wa Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi alitoa wito kuhakikisha juhudi za haraka zinahitajika ili kuongeza kasi katika utekelezaji wa itifaki ya biashara(2005) na soko la pamoja la SADC(2008).

 

Dk Stergomena licha ya kutotaja majina ya nchi, amesema juhudi hizo zinaenda sanjari na malengo ya uunganishaji masoko ya pamoja katika kanda tatu za Sadc, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) kabla ya soko la pamoja la bara la Afrika.

 

Advertisement

“Hali ya nchi kuridhia makubaliano ya soko la pamoja ya kanda hizo tatu bado hairidhilishi, Nchi 22 zimeshasaini makubaliano hayo, nchi 8 zimesharidhia zikiwamo tatu za Sadc. Katika makubaliano ya kuwa na soko la pamoja na Afrika, nchi 5 zimeridhia,” amesema Dk Stergomena. 

Katika mkutano huo wa matangazo mubashara kupitia teknolojia ya mtandao wa video kwa wajumbe wa nchi 16 wanaofuatilia, Dk Stergomena ameshauri kila nchi mwanachama kuridhia makubaliano ya soko la kanda hizo tatu muhimu zitakazochochea ukuaji wa kanda na bara hilo.

“Kwa sasa ni zaidi ya miaka 10 tangu kupitishwa makubaliano hayo mji wa Munyonyo nchini Uganda, bado hatujafanikiwa kuanza utekelezaji wake na muda unakwenda,” amesema. 

 

Advertisement