Dodoma haina shida ya vyakula

Muktasari:

Bei za mazao mkoani Dodoma zimepungua kutokana na wingi wa mazao hayo katika masoko mbalimbali.

Dodoma.Wingi wa mahindi na mazao mengine katika masoko mkoani Dodoma, umepunguza bei kutoka Sh70,000 kwa gunia la uzito wa kilo100 hadi Sh57,000 ikiwa ni pungufu ya Sh13,000.

Pia mchele unauzwa Sh170,000 hadi 200,000 kwa gunia la ujazo wa kilo 100 wakati mwaka jana msimu kama huu bei ilikuwa Sh190,000 hadi 240,000 kwa kipimo hicho.

Akizungumza na Mwananchi leo Oktoba 20, Kaimu meneja wa soko la mimataifa la mahindi Kibaigwa, Jonathan Mwashinga amesema hadi sasa wafanyabiashara wamejaza magodauni ya mahindi na pia uuzaji wake umekuwa chini ukilinganisha na mazao mengine kama mbaazi.

Amesema bei ya mbaazi kwa wastani wa gunia la kilo 100 imefikia Sh65,000 wakati mwaka jana msimu huu ilikuwa chini ya Sh50,000 na alizeti imefikia Sh1,000 kwa kilo huku ikiwa ni zao adimu linalotafutwa na wengi.

Mwanshinga ametolea mfano kuwa, wastani wa uingizaji mahindi katika soko hilo umekuwa ni tani 70 kwa siku wakati mbaazi zinaingizwa kwa wastani wa tani 270 kwa siku.

Ameeleza msimu wa mwaka huu watu walivuna mazao ya kutosha na kuwa mahindi yalianza kuingizwa sokoni Machi, hivyo inaonyesha hakutakuwa na upungufu wa chakula.

Ofisa masoko katika Jiji la Dodoma, Yuna James amesema hali ya upatikanaji wa vyakula bado ni ya kuridhisha, tofauti na ilivyokuwa mwaka jana huku akibainisha kuwa bei za vyakula pia ziko chini.

James amesema masoko yote ya Dodoma kuna nafaka ya kutosha na hajasikia malalamiko  yoyote.