Dovutwa apinga kuvuliwa uenyekiti UPDP, aitisha uchaguzi

Fahmi Dovutwa 

Muktasari:

Siku chache baada ya kuvuliwa uwenyekiti  wa chama cha UPDP, Fahmi Dovutwa ameibuka na kupinga uamuzi huo huku akiwataka wanachama wa chama hicho kujiandaa na uchaguzi.


Dar es Salaam. Siku chache baada ya kuvuliwa uwenyekiti  wa chama cha UPDP, Fahmi Dovutwa ameibuka na kupinga uamuzi huo huku akiwataka wanachama wa chama hicho kujiandaa na uchaguzi.

Desemba 2, 2019 makamu mwenyekiti wa chama hicho,  Abdallah Mohammed Khamis alitangaza Dovutwa kuvuliwa uwenyekiti kwa madai kutangaza kuwa UPDP haitashiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa uliofanyika Novemba 24, 2019.

Khamis amesema kauli hiyo ya Dovutwa imesababisha chama hicho kukosa wenyeviti wa Serikali za mitaa.

Akizungumza leo Alhamisi Desemba 5, 2019 Dovutwa amesema hajavuliwa uwenyekiti na wanaotangaza hivyo wana hofu ya uchaguzi wa chama hicho unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa Desemba, 2019.

"Niwatoe wasiwasi wanachama wa UPDP  waendelee na shughuli zao za ujenzi wa chama kwani kipo katika mikono salama ya mwenyekiti Dovutwa.”

"Chini ya uongozi wangu sijawahi kususia uchaguzi kwa kutamka wala ishara kwani uhai wa  UPDP ni kushiriki uchaguzi iwe kwa kushinda au kushindwa maana ni sehemu ya uchaguzi. Sitasusa na chama chetu ni huru hatushinikizwi na mtu yeyote kushiriki wala kususia,” amesema Dovutwa.

Akizungumzia habari za kuvuliwa uanachama, Dovutwa amesema walikuwa katika mkutano wa kawaida wa Halmashauri na katibu mkuu, Hamad Ibrahim alishinikiza Dovutwa kupigiwa kura kama amevunja au hakuvunja katiba ya chama hicho.

Dovutwa amesema mkutano wa halmashauri kuu ya chama hicho hauruhusiwi kumchukulia hatua yoyote, kwamba mwenyekiti ndio mwenye mamlaka ya kumwondoa madarakani kiongozi ambaye uchaguzi au uteuzi wake umefanywa na mkutano huo.

"Wanachama wote mjiandae na uchaguzi wa chama mwishoni mwa Desemba utakaofanyika mkoani Dar es Salaam. Maandalizi yake yameshakamilika. Msipokee taarifa mtu mwingine isipokuwa ofisi kuu za Dar es Salaam," amesema Dovutwa.