Dudubaya ajisalimisha Basata

Muktasari:

  • Siku 16 baada ya Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kumfutia usajili, msanii wa muziki wa kizazi kipya, Godfrey Tumaini maarufu Dudubaya amejisalimisha katika ofisi za baraza hilo zilizopo Ilala, Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Siku 16 baada ya Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kumfutia usajili, msanii wa muziki wa kizazi kipya, Godfrey Tumaini maarufu Dudubaya amejisalimisha katika ofisi za baraza hilo zilizopo Ilala, Dar es Salaam.

Januari 7, 2020 baraza hilo lilitangaza kumfungia Dudubaya kujihusisha na muziki baada ya kukaidi wito wa baraza hilo lililotaka kumhoji kuhusu tuhuma alizozitoa katika mitandao ya kijamii kuhusu tasnia ya muziki nchini.

Baraza hilo limesema wakati akieleza tuhuma hizo msanii huyo alitumia lugha isiyo na staha, aliitwa kuhojiwa kujua akilenga kitu gani.

Licha ya wito huo, msanii huyo hakuenda Basata na kueleza kuwa haoni kosa lake, huku akieleza mkakati wake wa kulipeleka baraza hilo mahakamani.

Kupitia video iliyopo katika ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Instagram wa baraza hilo, Dudubaya amesema ameamua kuonana na uongozi wa Basata kuzungumza nao kwa madai kuwa ndio wazazi wa wasanii.

"Basata ni wazazi wa wasanii, niliwapigia simu kuomba nionane nao na leo nimefanikiwa katika hilo. Tumeongea  mengi ambayo naamini yataleta  mabadiliko katika tasnia ya sanaa nchini," amesema Dudu Baya.