Watoto Ester na Eziekel wajishindia 120Mil East Africa Got Talent

Muktasari:

  • Ester na Ezekiel ambao ni ndugu kutoka Uganda wameibuka washindi katika mashindano ya East Africa Got Talent yaliyofanyika Kenya na kunyakua kitita cha dola za Kimarekani 50,000 (Sh120 milioni).

Dar es Saalam. Ni Jumapili ya baraka kwa wana-Afrika Mashariki baada ya shindano la kusaka vipaji Afrika mashariki (East Africa Got Talent) kumalizika kwa Ester na Ezekiel kuibuka washindi wa Dolla 50,000 za kimarekani.

Shindano la East Africa Got Talent msimu wa kwanza umemalizika leo Jumapili ya Oktoba 6, 2019 ambapo fainali zake zimefanyika nchini Kenya.

Katika fainali hizo washiriki sita walifika hatua ya fainali ambao ni  Jehova shallom, Intayoberana, DNA, Spelicast, Janell Tamara na Ester na Ezekiel.

Kwa mujibu wa kura zilizokuwa zikipigwa na watazamaji wa shindano hilo washiriki  Ester na Ezekiel waimbaji kutoka nchini Uganda walifanikiwa kuingia hatua ya tatu bora pamoja na  Intayoberana wacheza ngoma za asili kutoka Rwanda, Janell Tamara mwimbaji kutoka nchini Kenya.

Baada ya subira ya muda mrefu hatimaye aliyekuwa mshereheshaji wa shindano hilo Anne Kansiime aliwataja Ester na Ezekiel kuwa ndio washindi wa shindano hilo ambao wamejishindia kitita hicho cha fedha.

Shindano hilo ambalo ni mara ya kwanza kufanyika katika nchi za ukanda wa Afrika mashariki lilisimamiwa na majaji wanne ambao ni Jeff Koinange kutoka Kenya, Vanessa Mdee kutoka Tanzania, Makenda kutoka Rwanda, Gaetano Kongwa kutoka Uganda na Mshereheshaji Anne Kansiime kutoka Uganda.