Familia ya Balali yamwangukia Magufuli, yahangaika kutafuta mali alizoacha

Monday November 18 2019

 

By Ibrahim Yamola, Mwananchi iyam[email protected]

Dar es Salaam. Familia ya Gavana wa zamani wa Benki Kuu (BoT), Daud Balali imemuomba Rais John Magufuli kuisaidia kupata stahiki zao za nyumba, kiwanja na shamba, mambo ambayo imedai yanakwamishwa na baadhi ya watumishi serikalini.

Wamesema wamehangaika bila mafanikio kupata haki ya kiwanja namba 83 kilichopo Msasani jijini Dar es Salaam, shamba la Mbweni na nyumba iliyoko Masaki, huku wakiendelea kuishi maisha ya shida.

Familia hiyo inadai kuwa kiwanja hicho cha ekari mbili kilikuwa kinamilikiwa na mama yao, Rahel Vasolela aliyefariki dunia Februari 4, 2010 lakini kuna watu (majina tunayahifadhi baada ya kutopatikana) waliingilia kati kutaka kukichukua wakidai ni mali yao.

Balali alifariki dunia akiwa nyumbani kwake Maryland nchini Marekeani Mei 16, 2008. Alizikwa Mei 21 mwaka huo huo katika makaburi ya Gate of Heaven.

Wakizungumza na waandishi wa habari jana nyumbani kwa mama yao, Rahel Vasolela, Boko nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, wanafamilia hao walisema kifo cha ndugu yao kimegeuka mateso kwao kutokana na vitimbi wanavyofanyiwa.

Kuhusu kiwanja cha Msasani, Yasin Mjama, ambaye ni mpwa wa Balali, alisema kimekuwa na mgogoro baada ya mtu (jina tunalihifadhi) kudai ni chake licha ya hati alizonazo kuwa na utata.

Advertisement

“Walionyesha hati ambazo ziliibiwa nyumbani kipindi wezi walipokuja kuvunja nyumba na kuiba nyaraka mbalimbali ikiwamo hati hiyo,” alisema.

Alisema kutokana na utata huo, kamanda wa polisi wa kanda ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa aliwaagiza polisi ambao waliingilia kati kwa kuchukua maelezo na jalada kulipeleka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), lakini tangu liende ni zaidi ya mwaka ukimya umetawala.

“Sasa hatujui kwa nini jalada linakaa kwa DPP zaidi ya mwaka. Tukifuatilia wanakuwa wakali. Sasa tunataka kujua kuna nini kinaendelea,” alidai Mjama.

Baadaye Kamanda Mambosasa aliiambia Mwananchi kuwa wanaopaswa kuulizwa ni ofisi ya DPP.

Kuhusu muda wa jalada hilo kutoshughulikiwa, Mambosasa alisema: “Ni kweli limekaa muda mrefu. Sielewi kwa nini. Haiko sawa, limekaa muda mrefu mno.”

Hata hivyo, DPP Biswalo Mganga alisema: “Sifanyi kazi kwa mashinikizo, sawa? Tuache tufanye kazi.”

Mwanafamilia mwingine, Eva Balali (90) ambaye ni dada yao wa kwanza kuzaliwa, alisema anaadhirika kutokana na vitendo vya watu wanaowalalamikia.

“Sasa tunavyoona watu wa nje wanafanya uamuzi wa kubeba kila kitu. Kwa kweli tunaadhirika,” alisema.

“Tunaomba Rais atusaidie.”

Kwa upande wake, Magreth ambaye ni mdogo wa Balali alisema: “Tunaomba yeyote ambaye ana madai na Balali basi aje akae na familia hii. Sisi tupo, tuzungumze lakini sio kutuzunguka na kupita huko na huko kututesa.”

Alisema wakati Balali akiwa Gavana alikuwa akiishi katika nyumba ya Masaki, “na siku moja ilikuwa sikukuu ya Krismasi alitualika familia na siku ile alitueleza ‘hii nyumba nimeinunua ni yangu’ na sisi tukafurahi”.

“Alipokuwa akiumwa, nilikuwa nikiishia pale, lakini alipofariki, ghafla tu vitasa vikabadilishwa na tulipouliza tukaambiwa mna nyaraka. Sasa kwa kuwa hatukuwa na nyaraka tukashindwa,” alisema Magreth.

“Kwa hiyo tunamuomba Rais, yeye ni Rais wa wanyonge, aingilie kati ili kama nyumba ile ni ya kaka yetu tuelezwe. Kama ni ya Serikali tuelezwe kwa kuwa sisi kaka alituambia alishainunua nyumba hiyo.

“Tumehangaika sana. Tunamuomba Rais aingilie kati hili. Kuna watu wamechukua mali kwa kupora, waje hapa tujue kama ni mali za Rahel ama nani. Tumekaa sana na ndiyo maana tumeamua tuzungumze ili Watanzania wajue,” alisema.

Advertisement