Fatma Karume adai hukumu kuzuia wakurugenzi kusimamia uchaguzi ni kuzuia goli la mkono

Wakili Fatuma Karume akizungumza kwenye kongamano la vijana mkoani Arusha liliandaliwa na taasisi ya Change Tanzania. Picha Mussa Juma

Muktasari:

  • Rais mstaafu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume amesema uamuzi wa Mahakama Kuu kuwaengua wakurugenzi wa halmashauri  kusimamia  chaguzi mbalimbali nchini ni sawa na kuzuia goli la mkono katika uchaguzi.

Arusha. Rais mstaafu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume amesema uamuzi wa Mahakama Kuu kuwaengua wakurugenzi wa halmashauri  kusimamia  chaguzi mbalimbali nchini ni sawa na kuzuia goli la mkono katika uchaguzi.

Fatma ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Mei 24, 2019 jijini Arusha katika kongamano la taasisi ya Change Tanzania, akibainisha kuhusu hukumu hiyo ya kesi iliyofunguliwa na Bob Wangwe kwamba ina maana kubwa katika demokrasia ya Tanzania.

Hukumu hiyo ilitolewa Mei 10, 2019  na kuwaengua wakurugenzi hao wa halmashauri za majiji, miji/wilaya na manispaa kusimamia uchaguzi. Hata hivyo, Serikali imetia nia ya kukata rufaa kuhusu hukumu hiyo.

Wakurugenzi hao ambao wamekuwa wakilalamikiwa na vyama vya upinzani kuwa baadhi yao ni makada wa CCM, ndio wasimamizi wa uchaguzi kwa mujibu wa Sheria ya Taifa ya Uchaguzi kifungu cha 7(1).

Lakini, Mahakama Kuu katika hukumu yake pamoja na mambo mengine ilibatilisha kifungu hicho ikieleza kuwa kinakinzana na Katiba ya nchi Ibara za 21(1), (2) na ya 26(1), kuhusiana na ushiriki katika shughuli za uchaguzi na kutii na kufuata Katiba na sheria.

Hukumu hiyo ilitolewa na jopo la majaji watatu; Dk Atuganile Ngala (kiongozi wa jopo), Dk Benhajj Masoud na Firmin Matogolo kufuatia kesi ya kikatiba namba 17, ya mwaka 2018 iliyofunguliwa mahakamani hapo.

Akizungumzia hukumu hiyo leo,  Fatma amesema Watanzania wengi walikuwa wanajua jinsi wakurugenzi  wanavyovuruga uchaguzi lakini walikuwa kimya.

"Nimesaidia tumekwenda mahakamani tumeshinda kesi na hapa ndio tunaliondoa goli la mkono hivyo lazima tuungane" amesema.

Amesema ili kujua tatizo la wakurugenzi kusimamia uchaguzi ni vyema kutambua aliyewateua na sheria ya uchaguzi inasemaje.

"Kuna sheria ya Serikali za mitaa ambayo inazungumzia Rais kuteua wakurugenzi lakini kuna sheria ya uchaguzi ambayo inatambua hao wakurugenzi na kuwatumia.”

“Watu wanapenda kulalamika lakini hawachukui hatua ,tuige mfano wa Wangwe kwa kujitoa mhanga kufungua kesi hii,” amesema Fatma.

Kuhusu nia ya Serikali kukata rufaa, Fatma amesema kuna shinikizo la kisiasa tu na yeye kama wakili hana pingamizi kwani watakutana mahakamani.

Awali, wakili  Shilinde Swedi amesema ni muhimu vijana na jamii kuugana kudai haki na ikiwa ni pamoja na kufungua kesi za kimkakati kama alivyofanya Wangwe.

Wakili Swedi amesema change Tanzania ni fursa ya kuwaunganisha  vijana na watanzania katika kudai haki mbalimbali za kijamii.

Hukumu hiyo ilitolewa na jopo la majaji watatu; Dk Atuganile Ngala (kiongozi wa jopo), Dk Benhajj Masoud na Firmin Matogolo kufuatia kesi ya kikatiba namba 17, ya mwaka 2018 iliyofunguliwa mahakamani hapo.

Kesi hiyo ilifunguliwa na watetezi na wanaharakati wa haki za binadamu na demokrasia kwa kushirikiana na vyama vya siasa, kupitia kwa mwanaharakati Bob Wangwe dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Mkurugenzi wa Uchaguzi.

Pamoja na mambo mengine, Wangwe ambaye pia ni mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba alikuwa akidai kuwa wakurugenzi hao ni wateule wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye kwa sasa ndiye mwenyekiti wa CCM, chama ambacho pia hushiriki katika uchaguzi.

Alikuwa anadai kuwa hiyo ni kinyume cha Ibara ya 74 (14 ) ya Katiba ya nchi ambayo inapiga marufuku kwa mtu yeyote anayehusika na uchaguzi kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa na kwamba ana haki ya kupiga kura tu.

Katika kuweka uzito madai yake, Wangwe aliyekuwa akiwakilishwa na Fatma aliwasilisha mahakamani hapo orodha ya majina ya wakurugenzi 73 na ushahidi kuwa ama ni makada wa CCM au waliwahi kushiriki katika kugombea au kuomba kugombea nafasi mbalimbali kupitia chama hicho.

Wakati ikitoa uamuzi wake Mahakama ilisema kuwa imeridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo kuwa orodha ya majina ya wakurugenzi hao ni wanachama wa CCM kwa kuwa Serikali ilishindwa kuthibitisha kuwa si wanachama wa CCM.

Mahakama hiyo ilisema kuwa jambo hilo linaweza kuathiri utendaji kazi wao wa uhuru na haki kutokana na kuwa na maslahi na chama hicho, kinyume cha matakwa ya katiba ambayo inataka tume hiyo iwe huru katika kutekeleza majukumu yake.