Fedha alizozidai Mbunge Keissy zaota mbawa, Ndugai atoa sababu

Muktasari:

Malengo yaliyowekwa na Umoja wa Wabunge Wanawake Tanzania (TWPG) ya kujenga choo kimoja cha mfano kwa kila jimbo nchini humo yameshindwa kufanikiwa na badala yake fedha zilizokuwa zimekusanywa kwa lengo hilo zitatumika kujenga Shule ya wasichana jijini Dodoma ambayo itapewa jina la TWPG Girls.

Dodoma. Mpango wa ujenzi wa vyoo bora uliokuwa ukipigiwa debe na wabunge wanawake wa Bunge la Tanzania umeota mbawa na sasa wanajenga shule.

Bunge la Tanzania lilifanya makongamano mawili katika majiji ya Dar es Salaam na Dodoma na kufanikiwa kuchangia Sh1.22 bilioni na ahadi ya Sh383 milioni lengo likiwa ni kukenga vyoo vya mfano kwa ajili ya wasichana kwa kila jimbo nchini humo.

Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai ametangaza bungeni leo Ijumaa Septemba 13, 2019 wakati akiahirisha mkutano wa 16 wa Bunge jijini Dodoma.

Amesema fedha hizo zitajenga Shule ya wasichana katika Jiji la Dodoma ambayo itaitwa TWPG Girls ambayo itachukua wanafunzi kidato cha kwanza hadi cha nne.

TWPG ni Umoja wa Wabunge Wanawake Tanzania.

Tangazo la Ndugai ambalo lilionekana kupingwa na sauti za wabunge wanawake kwa sauti za hapana, ilionyesha Serikali haiwezi kuendelea kuwa na fedha hizo ambazo msingi wake umeshindwa kufikiwa.

Katika mkutano uliopita, Mbunge wa Nkasi (CCM) Ally Keissy alihoji juu ya fedha hizo akisema kuna mashaka huenda zimeliwa na kama zipo akataka wagawane kila mtu achukue chake lakini Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson aliyekuwa amekalia kiti siku hiyo akasema Spika ndiye mwenye majibu.

Licha ya kelele zakupinga lakini Spika Ndugai amesisitiza ulikuwa msimamo wa wabunge wanawake kwa ajili ya kuweka kumbukumbu kwani kiasi kilichopatikana hakiwezi kutosheleza malengo yao.