Foden aikoa Man City England

Muktasari:

Hadi sasa mabingwa hao wa zamani wa soka England wameambulia pointi moja katika mechi nne za Ligi Kuu na tayari wako nyuma ya vinara Leicester kwa tofauti ya pointi tano.

London, Uingereza (AFP). Pep Guardiola amekiri kuwa hawezi kuwa na uhakika kuwa Manchester City itazinduka kutoka katika matokeo mabaya baada ya Phil Foden kutokea benchi na kuiwezesha kupata sare ya bao 1-1 na West Ham katika mechi ya Ligi Kuu ya soka ya England leo Jumamosi.

Timu ya Guardiola iliruhusu bao katika kipindi cha kwanza wakati Michail Antonio alipoufuata mpira wa juu na kupiga kiki kuandika bao la kuongoza katika Uwanja wa London.

Foden aliingizwa uwanjani katika kipindi cha pili na akafunga bao la kusawazisha, lakini City haikuweza bao la jingine ugenini na sasa imeshinda mechi moja kati ya nne za Ligi Kuu.

City, ambayo imekumbwa na tatizo la majeruhi, ikiwakosa Fernandinho, Aymeric Laporte, Nathan Ake na Gabriel Jesus, ilifikia kwa nadra kiwango chake cha ubora katika mechi hiyo iliyoongeza matokeo mabovu kwa timu hiyo.

City bado haionekani kuwa imerejea katika hali yake baada ya kubugizwa mabao 5-2 na Leicester mwezi uliopita.

Tayari iko nyuma kwa tofauti ya pointi tano kwa vinara Everton, ambao kesho Jumapili watakutana na Southampton, na ilionekana mbovu kuliko wakati wowote tangu msimu wa kwanza wa Guardiola katika klabu hiyo.

"Mimi si mtu ambaye anaweza kubashiri hali ya baadaye. Tumeshapoteza pointi saba, ambazo ni nyingi,"  alisema Guardiola.

"Tulikuwa na wakati mgumu katika dakika 10 au 15 za kipindi cha kwanza. Kipindi cha pili tulikuwa vizuri na tulifunga mwanzoni.

"Tulipata nafasi zilizotakiwa kushinda mchezo, lakini bahati mbaya hatukuweza kufunga tena.

"Tumesumbuka sana kwa sababu nyingi. Hatuna budi kujifunza katika kila mechi na kuona nini kitatokea."

Kuongezea katika matatizo ya Guardiola, Sergio Aguero alipata matatizo ya misuli, kwa mujibu wa kocha huyo, ambaye hakujua itamchukua muda gani mshambuliaji huyo nyota kurudi uwanjani.

Aguero hajafunga bao katika mechi za Ligi Kuu tangu Januari na imemchukua muda kurejea katika ubora wake baada ya majeraha.

Akiwa ndio kwanza amerejea uwanjani baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti, mshambuliaji huyo wa Argentina alibadilishwa wakati wa mapumziko na nafasi yake kuchukuliwa na Foden.

Safari ngumu ya kwenda Marseille na baadaye Sheffield United wiki ijayo, itampa mtihani mwingine wa jinsi gani City itatengemeaa kurejea katika ubora wake ulioipa ubingwa mwaka 2018 na 2019.

Baada ya kuzinduka kutoka katika uwezekano wa kulala kwa mabao 3-0 katika dakika kumi za mwisho za mechi iliyopita, haya ni matokeo mengine ya kuridhisha kwa West Ham.

Raheem Sterling alifunga mabao matatu dhidi ya West Ham wakati City iliposhinda kwa mabao 5-0 msimu uliopita na mbio zake kupenya kwa mabeki zilimtengenezeanafasi nzuri Aguero, ambaye shuti lake lilimgonga beki na kutoka nje.