Gumzo mabadiliko ya CAG

Monday November 04 2019
pic gumzo

Dar es Salaam. Baada ya kuteuliwa mara tatu ndani ya miaka minne kushika nyadhifa mbalimbali, Charles Kichere amefika kikomo cha uteuzi.

Jana, Rais John Magufuli alitangaza kumteua Kichere kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), nafasi ambayo Katiba ya nchi inazuia mhusika kuteuliwa tena katika nafasi yoyote atakapomaliza utumishi wake.

Ibara ya 144 (6) inasema, “mtu aliyepata kuwa CAG hawezi kuteuliwa kushika madaraka ya kazi nyingine yoyote katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.”

Si hilo tu, uteuzi wa Kichere na kuachwa kwa Profesa Mussa Assad ambaye ndiye CAG anayemaliza kipindi chake cha kwanza cha miaka mitano leo kumezua gumzo nchini na katika mitandao ya kijamii.

Kuanzia mwaka 2016 hadi jana, Kichere alikuwa ameteuliwa mara tatu na Rais Magufuli kushika nafasi tofauti, akipandishwa cheo mara mbili na ‘kushushwa’ mara moja.

Akiwa mkaguzi wa ndani wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Kichere aliteuliwa kuwa naibu kamishna mkuu wa Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA), Novemba 2016, nafasi aliyohudumu kwa mwaka mmoja kabla ya kupandishwa cheo na kumrithi aliyekuwa kamishna mkuu wa mamlaka hiyo, Alphayo Kidata aliyeteuliwa kuwa katibu mkuu Ikulu, Novemba, 2017.

Advertisement

Kichere alidumu kwenye nafasi hiyo mpaka Juni 8, mwaka huu alipopelekwa mkoani Njombe kuwa katibu tawala wa mkoa (Ras).

Kwa uteuzi huu mpya wa kuwa CAG, Kichere amemalizana na mamlaka ya uteuzi.

Kichere anakuwa mtu wa saba kushika wadhifa wa CAG tangu nchi ipate uhuru mwaka 1961.

Kwenye majukumu yake mapya yanayoainishwa na Ibara ya 143 (2), Kichere anaenda kuhakikisha matumizi ya fedha zote zinazotolewa kwenye mfuko mkuu wa Serikali yameidhinishwa na kufanya ukaguzi na kutoa taarifa juu ya ukaguzi wa hesabu za Serikali.

Katika kutekeleza majukumu hayo, Katiba inaagiza kuwa CAG hatalazimika kufuata amri au maagizo ya mtu mwingine yeyote au idara yoyote ya Serikali.

Kichere (50) ataendelea na majukumu hayo mpaka ukomo wake utakapofika kwa mujibu wa Katiba inayoelekeza kuwa “CAG atalazimika kuacha kazi yake atakapotimiza umri wa miaka sitini au umri mwingine wowote utakaotajwa na sheria iliyotungwa na Bunge.”

Kichere aliondolewa TRA, siku moja baada ya Rais Magufuli kukutana na wafanyabiashara kutoka halmashauri zote nchini mwaka huu.

Kwenye mkutano huo uliofanyika Juni 7 mwaka huu, Ikulu jijini Dar es Salaam, wafanyabiashara hao walilalamikia vitisho wanavyopewa na maofisa wa TRA wanapokwenda kukusanya mapato ya Serikali, kuombwa rushwa na unyanyasaji.

Kero nyingine zilizoelezwa ni uwapo wa tozo zenye kero zinazokatisha tamaa wafanyabiashara na wawekezaji.

Kwenye hotuba yake kabla ya kumwondoa Kichere, Rais Magufuli alisema alikuwa anapokea malalamiko mengi ya wafanyabiashara na kila ujumbe mfupi wa maneno aliokuwa anatumiwa alikuwa anaupeleka kwa Kichere, lakini hakuna hatua alizokuwa anachukua.

“Huwa anapokea na kusema amepata, lakini hakuna anachofanya,” alisema Rais Magufuli wakati huo.

Profesa Assad

Kichere anarithi mikoba ya Profesa Assad aliyeteuliwa kushika wadhifa huo, Novemba 5, 2014 na leo anatimiza miaka mitano.

Profesa Assad aliyezaliwa Oktoba 6, 1961 alichukua nafasi hiyo baada ya Ludovick Utouh kustaafu.

Professa Assad anapumzika ikiwa ni miezi 10 tangu ahojiwe na Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge Januari 21 kwa kufanya mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya redio ya Umoja wa Mataifa (UN) jijini New York Desemba 2018 na kuliita Bunge ‘dhaifu’.

Katika mahojiano hayo alisema Bunge la Tanzania halina meno na limeshindwa kuiwajibisha ipasavyo Serikali.

Kutokana na mgogoro uliokuwepo, Spika wa Bunge, Job Ndugai aliweka bayana kuwa Bunge haliko tayari kufanya kazi na Profesa Assad.”

Msimamo huo wa Ndugai ulitokana na Azimio la Bunge lililopitishwa Aprili 2, mwaka huu likielekeza kutofanya kazi na Profesa Assad.

Kwa mujibu wa Sheria ya Ukaguzi wa Hesabu za Umma ya mwaka 2008, mtu anayeteuliwa kuwa CAG anatakiwa kuhudumu kwenye nafasi hiyo kwa muhula wa miaka mitano huku kukiwa na uwezekano wa kuongezewa muhula mwingine zaidi.

Endapo mtu huyo atatakiwa kustaafu, sheria inasema ni pale atakapotimiza miaka 65 au akimwandikia barua Rais wa Tanzania kumuomba kupumzika. Barua hiyo inatakiwa kuandikwa miezi sita kabla ya siku ya kuondoka ofisini.

Kwa muda wa utumishi wake, Profesa Assad anakamilisha muhula mmoja leo tangu alipoanza kutekeleza majukumu ya mdhibiti na mkaguzi mkuu Novemba 5, 2014.

Alipotafutwa kupata maoni yake jana, Profesa Assad alisema: “Usiogope kupoteza riziki yako kwa sababu Mungu ndiye mpaji na utoaji wake hauna kikomo. Ninamshukuru Mungu kwa kila kitu.”

Wabunge wanena

Baadhi ya wabunge waliozungumzia uteuzi wa Kichere kuwa CAG mpya wamesema watashirikiana naye kwa mujibu wa sheria ila wakamtaka kutekeleza majukumu yake kwa weledi na uzalendo.

Naibu waziri kivuli wa Fedha na Mipango, David Silinde alisema wanasubiri kuona ufanisi wake.

“Hakuna namna sisi tutafanya naye kazi kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake,” alisema.

Ingawa sheria inaruhusu CAG kuongezewa muhula mwingine wa miaka mitano au kustaafu akifikisha miaka 60 kama Katiba ya nchi inavyoelekeza, Silinde alisema hajui kwa nini Rais ameamua kumpumzisha Profesa Assad baada ya kukamilika muhula wake wa kwanza.

“Hii ni mara ya kwanza kutokea ingawa Rais ametumia mamlaka aliyonayo kikatiba,” alisema mbunge huyo wa Mbozi kwa tiketi ya Chadema.

Mbunge wa Iramba Mashariki (CCM), Allan Kiula alisema ofisi ya CAG ni kubwa sana na wananchi wanaitegemea kufahamu matumizi ya fedha zao.

Kuhusu uteuzi huo alisema hana wasiwasi kwani taarifa ya Ikulu imeeleza vizuri kwamba utumishi wa Profesa Assad unakamilika leo hivyo ni lazima awepo mtu wa kuchukua nafasi yake.

Kwenye taarifa ya chama chake cha ACT Wazalendo, mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe alisema Sheria ya Taifa ya Ukaguzi ya mwaka 2008 inatoa vipindi viwili vya miaka mitano kwa CAG kukaa madarakani isipokuwa akitimiza miaka 65 na ni lazima ahudumu kwa mihula miwili.

“CAG wa Tanzania kwa mujibu wa Katiba ni Profesa Mussa Assad hadi mwaka 2024,” alisema Zitto.

Advertisement