Gurdiola aivulia kofia Liverpool

Muktasari:

  • Pep Guardiola amesema pengo la pointi baina yao na Liverpool ni kubwa na wapinzani wao hawatakubali kuachia pointi katika mechi zao zijazo.

London, England. Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola amesema pengo la pointi baina yao na Liverpool ni kubwa.

Liverpool inaongoza ligi kwa pointi 24 na Man City inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 16 baada ya kufungwa mabao 2-0 na Wolves.

Timu hizo ambazo zinakabana koo kuwania ubingwa wa Ligi Kuu zina tofauti ya point inane.

Hata hivyo, alisema ana vijana wapambanaji ambao wataivusha Man City katika kipindi hicho kigumu.

“Nawafahamu vijana wangu ni wapiganaji. Wana nafasi ya kupambana na kuiweka sawa timu,”alisema kocha huyo wa zamani wa Barcelona na Bayern Munich.

Liverpool imeonekana kuwa katika kiwango bora kwa asilimia 100 na juzi ilipata ushindi licha ya bao lake la penalti kuibua utata dhidi ya Leicester City.

“Katika mazingira yoyote Liverpool haitakubali kupoteza pointi. Lakini hatuwezi kukata tamaa huu ni mwezi Oktoba tuna idadi kubwa ya mechi zimebaki,”alisema Guardiola.

Miamba hiyo inatarajiwa kuvaana Novemba 10 katika mchezo ambao utatoa taswira ya timu gani itakuwa na nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa msimu huu.

Man City inapambana kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya tatu mfululizo tangu Man Manchester United ilipotwaa msimu 2007-2009.