HABARI MAALUMU: Wahadzabe wanavuna mamilioni kila mwaka kwa kuuza ‘hewa’-1

Friday September 20 2019

 

By Florence Majani

Je unajua kuwa hewa inauzwa? Unafahamu kuwa hewa hiyo ikiuzwa inaweza kukupatia mamilioni ya fedha?

Kama hujui basi hivyo ndivyo jamii ya Wahadzabe, wanaoishi katika vijiji vya Domanga, Mongo wa Mono na Yaeda Chini wilayani Mbulu mkoani Manyara wanavyopata mamilioni ya fedha kila mwaka kwa kuuza hewa.

Jamii ya Wahadzabe hao inapata kiasi cha Sh150 milioni kila mwaka kwa kutokata misitu yao na hivyo kuendelea kuzalisha hewa safi.

Wanapata fedha hizo kupitia mradi wa Carbon Tanzania kwa kushirikiana na Taasisi ya Tanzania Nature Conservancy ambao kazi yao ni kuwaelimisha Wahadzabe kuhusu utunzaji misitu na baada ya hapo, mataifa makubwa duniani yanayozalisha hewa chafu za viwandani, hutoa fedha kwa jamii zinazotunza misitu.

Akizungumza na Mwananchi, muasisi wa Carbon Tanzania, Mark Baker anasema, kuuzwa kwa hewa hiyo hakuhitaji magari au mitambo ya kuibeba sehemu moja kwenda nyingine, bali ni mchakato wa mataifa makubwa yanayofanya shughuli za uchafuzi wa hewa kutoa fedha kwa jamii inayotunza misitu inayonyonya hewa chafu.

“Sisi Carbon tunashirikiana na jamii, mfano hawa Wahadzabe kuwaelimisha ili wasikate misitu na wawe na mipango sahihi ya matumizi ya ardhi, kitendo hicho pekee kinazalisha hewa safi na ile miti inanyonya hewa ya ukaa Kaboni dayoksaidi (CO2) inayozalishwa na magari, ndege na kwenye viwanda,” anasema.

Advertisement

Baker anasema baada ya kuelimishwa, jamii ya Wahadzabe iliingia mkataba wa miaka 20 na Carbon Tanzania na kukubaliana kuhusu mipango sahihi ya matumizi ya ardhi, mfano kutenga ardhi ya malisho ya mifugo, kilimo na ardhi ya hifadhi kwa ajili ya kutunza misitu. “Kwa kufanya hivi, sisi Carbon tunaratibu ni kiasi gani cha hewa kilichozalishwa kwenye miti hii na kisha kuuza kwa mataifa makubwa,” anasema.

Anasema mataifa hayo, hutoa fedha kama fidia kutokana na shughuli za kila siku zinazosababisha uchafuzi wa mazingira ambazo asilimia 40 huchukuliwa na Carbon na asilimia 60 hupelekwa kwa jamii ya Wahadzabe ambao hujipangia namna ya kuzitumia.

“Kila tani ya Carbon inatathminiwa kwa thamani ya dola. Tani hiyo ya Carbon huuzwa na mapato yake hugawawiwa kwa jamii ya Wahadzabe,” anasema Baker.

Mchakato huu wa mataifa makubwa kutoa fedha kwa jamii zinazotunza misitu ulitokana na mkataba wa Paris wa mwaka 2015.

Makubaliano ya mkataba huo ni pamoja na kwa namna gani nchi zitatoa ripoti kuhusu kiwango cha gesi chafu katika mataifa yao na juhudi za kuipunguza, hakikisho la ufadhili wa kifedha kwa mataifa maskini ili kusaidia kupunguza gesi ya Carbon, kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi yasiyoepukika pamoja na mataifa makubwa kulipa kwa ajili ya uharibifu ambao tayari umetokea.

Kwa nini Wahadzabe?

Baker anasema, Wahadzabe walichaguliwa kuwa sehemu ya mradi huu ulioanza mwaka 2010 kwa kuwa wao tayari wana mila na taratibu za utunzaji wa mazingira.

“Kiasili wanategemea misitu na wanyama pori katika maisha yao, chakula chao ni matunda ya asili, mizizi na wanyama, hivyo ilikuwa rahisi kuwapa elimu ya kuwa wakitunza hii misitu basi wataendelea kupata chakula chao cha kila siku, na kweli wamefanikiwa,” anasema.

Baker anaongeza kuwa kama Tanzania inataka kumaliza uharibifu wa misitu, watu wanaoishi vijijini wanapaswa kupata msaada wa kifedha. Hicho ndicho Carbon inachofanya,” anasema.

Ili kujua kama eneo husika halijaharibu misitu na kubaini kiasi cha hewa chafu kilichonyonywa na misitu hiyo, Carbon hutumia teknolojia ya satellite.

“Picha za satellite huchukuliwa na kuona hali ya misitu katika eneo hilo, pia kupima tani za hewa safi zilizozalishwa,” anasema.

Ofisa Usimamizi wa Mazingira wa Halmashauri yaWilaya ya Mbulu, Kilimba Kingu anasema fedha zinazopatikana kwa utunzaji misitu kila mwaka hugawanywa kwa vijiji vitatu ambavyo ni Domanga, Mongo wa Mono na Yaeda Chini.

“Kila kijiji kinapata Sh25 hadi 28 millioni kila baada ya miezi sita, hizo fedha hutengwa kulingana na mahitaji muhimu ya jamii za Wahadzabe, kwa mfano kiasi hununuliwa mahindi, nyingine huwekwa kwenye elimu, na nyingine kwa ajili ya afya.

Ofisa Mradi wa Carbon Tanzania, anayeratibu utunzaji wa misitu kwa jamii ya Wahadzabe, Isaack Magombe anasema, fedha zinazowekwa katika afya zinapelekwa moja kwa moja katika Hospitali ya Hydom iliyopo eneo hilo.

“Hivyo Wahadzabe wanapougua, huenda hospitali na kupata matibabu bure, ni kama bima ya afya ya jumla kwa Wahadzabe wote,” anasema

Magombe anasema jamii ya Wahadzabe wenyewe ndio huamua kiasi gani cha fedha kipelekwe katika elimu, afya na katika chakula.“Kwa mfano katika miezi sita ya Januari hadi Juni mwaka huu, hawajanunua chakula kwa sababu mahitaji ya elimu yalikuwa makubwa,” anasema.

Ili kuhakikisha hakuna anayeharibu mazingira, Jamii ya Wahadzabe imeajiri vijana 13 katika kijiji cha Domanga kwa ajili ya kufanya doria mara mbili kwa wiki katika maeneo ya hifadhi.

Katika vijiji vyote vitatu, Domanga, Mongo wa Mono na Yaeda Chini, kuna askari wa doria 42.

Itaendelea kesho...

Pili Goodo, mratibu wa vijana wa ulinzi wa jamii ya Wahadzabe, anasema ili kusimamia maeneo ya misitu yasiharibiwe askari wa vijiji walitafutwa.

“Hawa kazi yao ni kuangalia ‘beacon’ zisiharibiwe, miti isikatwe, kupambana na majangili,” anasema na kuongeza kuwa kila askari hulipwa Sh80,000 kwa mwezi kwa kazi hii ya kulinda misitu.

Mwenyekiti wa bodi ya Elimu wa Wahadzabe, Ezekiel Philipo anasema asilimia 25 ya fedha (sawa na Tsh4milioni kila baada ya miezi sita) huwekwa kwenye elimu.

“Yaani kutokana na huu utunzaji wetu wa misitu, sasa watoto wa Kihadzabe wanasoma bure, kuanzia shule ya msingi na hata wanapoingia sekondari wanapewa mahitaji muhimu,” anasema.

Anasema fedha hizo zinawasaidia wanafunzi kupanga vyumba karibu na shule, kununua vitanda, magodoro na fedha za kujikimu kwa chakula.

“Wakati mwingine hizi fedha zinatumika kujenga vyumba vya madarasa na kusaidia masuala mengine ya elimu,” anasema Philipo.

Mkurugenzi wa halmashauri ya Mbulu, Hudson Kamoga anawashukuru watu wa Carbon kwa kuwapa elimu jamii ya Wahadzabe kutunza misitu na kufaidika na mamilioni hayo kila mwaka.

Anasema kuna kiasi cha fedha kinachotengwa kwa ajili ya shughuli za utunzaji wa misitu zinazofanywa na Halmashauri hiyo.

Itaendelea kesho

Advertisement