Habari njema kwa wakulima wa mbogamboga, maua nchini Tanzania

Wednesday August 14 2019

 

By Mussa Juma, Mwananchi [email protected]

Arusha. Wakulima wa mbogamboga na maua nchini Tanzania waliokuwa wakipata hasara kutokana na  kushindwa kuhifadhi kwa muda mrefu mazao yao sasa wataanzania kuwa na nyuso za furaha.

Ni kutokana na tume ya nguvu za Atomic kuja na mradi wa kiwanda cha mionzi ya kuhifadhi maua na mbogamboga.

Kiwanda hicho kinatarajiwa kugharimu Sh4 bilioni na kitajengwa mkoani Arusha ambako kuna uzalishaji mkubwa wa maua na mbogamboga

Mtafiti mwandamizi wa tume hiyo, Yesaya Sungita akizungumza na Mwananchi amesema mradi wa kiwanda hicho tayari umeandikwa na kufikishwa serikalini.

“Tunatarajia mradi huu ukipitishwa na Serikali na kupatikana fedha, kitajengwa viwanda mkoani Arusha na kingine jijini Dar es Salaam,” amesem

Amebainisha kuwa kama mradi huo ukipitishwa na kupatikana fedha ndani ya miaka minne , kiwanda cha kwanza kinaweza kuwa kimekamilika na kusaidia sekta ya maua na mbogamboga.

Advertisement

"Afrika Kusini, Nigeria  na Misri wana viwanda vya aina hii na vimekuwa na faida kubwa kwa wakulima wa mbogamboga na maua,” amesema.

Wakizungumza mradi huo, baadhi ya wakulima wa maua na mbogamboga, wameshukuru tume hiyo kwa kuja na mradi huo utakaosaidia kuwapunguzia hasara.

Jane Minja, mkulima wa mbogamboga eneo la Tengeru wilayani Arumeru, amesema kwa muda mrefu wamekuwa wakipata hasara ya mboga kuharibika kabla ya kusafirishwa.

“Mbogamboga na maua vina soko zaidi nje ya nchi sasa kama huwezi kuhifadhi kabla ya kusafirisha utapata hasara,” amesema.

Naye Peter Pendaeli amesema hulazimika kusafirisha maua nchini Nairobi ili kupata ndege zinazokwenda moja kwa moja barani Ulaya, kwamba ujio wa viwanda hivyo ni nafuu kwao

Advertisement