Hakielimu wataja sababu wanafunzi kufeli

Muktasari:

  • Wazazi na walezi kutowahamasisha watoto wao kufanya vizuri katika masomo ni moja ya sababu ya baadhi ya wanafunzi katika mikoa mbalimbali nchi kufanya vibaya katika mitihani ya kumaliza elimu ya msingi mwaka 2019

Dar es Salaam. Wazazi na walezi kutowahamasisha watoto wao kufanya vizuri katika masomo ni moja ya sababu ya baadhi ya wanafunzi katika mikoa mbalimbali nchi kufanya vibaya katika mitihani ya kumaliza elimu ya msingi mwaka 2019.

Mikoa iliyofanya vibaya matokeo ya darasa la saba kwa miaka mitano mfululizo kuanzia mwaka 2019 ni Singida, Dodoma, Mtwara, Mara, Tanga, Kigoma, Tabora na Manyara.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Januari 22, 2020 katika uzinduzi wa ripoti ya utafiti kuhusu mikoa iliyofanya vizuri na ile iliyofanya vibaya katika matokeo ya darasa la saba, mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya Hakielimu, Dk John Kalage amesema utafiti huo ukitumiwa utaboresha ufaulu.

“Utafiti huu uliwashirikisha wazazi, walimu wakuu, wakuu wa bodi za shule na wanafunzi. Tumegundua kuna changamoto ya miundombinu kutoka Mkoa mmoja kwenda mwingine, umbali mrefu kutoka nyumbani kwenda shule hali inayosababisha walimu na wanafunzi kuingia darasani wakiwa na uchovu,” amesema.

Dk Kalage amesema mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Geita, Iringa, Kilimanjaro  na Kagera imefanya vizuri katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba kwa miaka mitano mfululizo.

Amesema Mikoa hiyo imefanya vizuri kutokana na kuwa na ubora katika uongozi na menejimenti, kuanzia katika Wilaya hadi shule husika.

Amesema sababu nyingine ni mbinu za ziada kuimarisha ufundishaji.

“Lakini pia tumegundua katika mikoa hii kuna ushiriki wa wazazi na mahusiano mazuri na walimu pamoja na hamasa kwa walimu,” amesema.

Ameongeza, “HakiElimu kama shirika linalounga mkono juhudi za Serikali  kutoa elimu yenye ubora na usawa, tungependa kuona kila Mkoa ukifanya vizuri kila mwaka ili kuwa na uhakika kwa watoto wengi zaidi wanapata fursa ya kufaulu na kuendelea na masomo.”

Mtafiti wa Shule ya Elimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Shukia amesema ni vyema mikoa ambayo haifanyi vizuri  katika mitihani ya darasa la saba kuiga katika mikoa iliyofanya vizuri ili kuinua kiwango cha elimu.