Hakimu ahimiza upelelezi kesi ya Dk Ringo Tenga

Friday March 1 2019

By Pamela Chilongola,Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Thomas Simba ameutaka upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi ili kesi inayowakabili vigogo wa kampuni ya Mawasiliano ya Six Telecoms Limited, akiwemo wakili Dk Ringo Tenga, iweze kuisha haraka.

Hatua hiyo imekuja baada ya Wakili wa Serikali, Jacquline Nyatori kuieleza mahakama hiyo, kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado haujakamilika.

"Jalada lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kwa ajili ya kuandaa huo ushahidi kazi ambayo ilishaanza na umefikia hatua nzuri kwa jinsi nilivyoona safari ijayo tunaweza kuja na lugha nzuri," alidai Nyatori.

Hakimu Simba alisema kesi hiyo ni ya muda mrefu hivyo ifike mwisho tunataka lishughulikiwe haraka ili shauri hilo liweze kuisha mapema.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Machi 15, 2019 itakapotajwa tena na washtakiwa wamerudishwa rumande kwa kuwa shtaka linalowakabili halina dhamana.

Mbali na Dk Tenga, washtakiwa wengine ni Hafidhi Shamte au Rashidi Shamte ambaye ni mkurugenzi mkuu wa kampuni wa hiyo, mfanyabiashara na mkurugenzi wa kampuni hiyo, Peter Noni, mkuu wa fedha wa kampuni hiyo Noel Chacha na Kampuni ya Six Telecoms.

Advertisement

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka sita yakiwemo ya utakatishaji fedha.

Katika kesi ya msingi, Dk Ringo ambaye ni mkurugenzi na mwanasheria wa kampuni hiyo na wenzake wanadaiwa kuwa, kati ya Januari 1, 2014 na Januari 14, 2016 Dar es Salaam, walitoza maalipo ya mawasiliano ya simu za kimataifa chini ya kiwango cha Dola za Marekani 0.25 kwa dakika kwa lengo la kujipatia faida.

Pia katika kipindi hicho, wanadaiwa kuhujumu miundombinu ya Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) kwa kutoza gharama chini ya kiwango na kushindwa kulipa Dola za Marekani 3,282,741.12 kwa TCRA, kama malipo ya mapato.

Washtakiwa hao wanadaiwa katika kipindi hicho walishindwa kulipa ada za udhibiti za Dola za Marekani 466,010.07 kwa TCRA.

Katika shitaka la utakatishaji fedha, Hafidhi, Noni, Tenga na Chacha, wanadaiwa kuwa walitumia ama walisimamia Dola za Marekani 3,282,741.12 wakati wakijua fedha hizo ni zao la makosa ya udanganyifu linalotokana na mashitaka yaliyotangulia.

Vile vile washitakiwa hao wanadaiwa kuwa waliisababishia TCRA hasara ya Dola za Marekani 3,748,751.22 (sawa na Sh. 8bilioni ).


Advertisement