Hakimu amtaka shahidi kesi ya Mpemba wa Magufuli

Monday September 16 2019

 

By Pamela Chilongola na Rebeca John mwananchipapers @mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Thomas Simba ameutaka upande wa mashtaka katika kesi ya  uhujumu uchumi inayomkabili, Yusuf Ali Yusuf, maarufu  ‘Mpemba wa Magufuli’ kuhakikisha shahidi anayetakiwa kutoa ushahidi anakuwepo mahahakamani hapo shauri hilo litakapokuja kwa ajili ya kusikilizwa.

Hatua hiyo imekuja baada ya Wakili wa Serikali, Omary Msemo kudai mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa shahidi waliyekuwa wakimtegemea kutoa ushahidi amepata dharura.

"Kwa bahati mbaya shahidi tuliyemtegemea kuja leo amepata dharura asubuhi hii, hivyo naiomba mahakama hii ipange kesho tuendelee na ushahidi,"alidai Msemo.

Hakimu Simba alisema hakikisheni shahidi anakuwepo ili shauri hilo liweze kuendelea mbele hivyo kesi hiyo itaanza kusikilizwa Septemba 17, 2019 saa 4 asubuhi.

Mbali na Yusuph, washtakiwa wengine katika kesi hiyo  ni Charles Mrutu, maarufu kama Mangi Mapikipiki na mkazi wa Mlimba, Morogoro; Benedict Kungwa, mkazi wa Mbagala Chamazi;  Jumanne Chima, maarufu kama JK na mkazi wa Mbezi;  Ahmed Nyagongo, dereva na mkazi wa Vikindu-Mkuranga na Pius Kulagwa, mfanyabiashara na mkazi wa Temeke.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka manne, likiwemo la kujihusisha na mtandao wa ujangili, katika kesi ya uhujumu uchumi namba 53/2016.

Advertisement

Miongoni mwa shtaka moja kati ya manne yanayowakabili washtakiwa hao ni kujihusisha na mtandao wa ujangili kwa kukusanya na kuuza nyara za Serikali ambazo ni vipande 50 vya meno ya tembo vyenye thamani ya dola 180,000 sawa na Sh 392,817,600 bila kuwa na kibali cha mkurugenzi wa wanyamapori.

Advertisement