Hakimu ashitaki vyombo vya mahakama vilivyomfuta kazi

Wednesday November 20 2019

 

By James Magai, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Aliyekuwa Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kalambo, mkoani Rukwa, Jonathan Ernest Mgongoro ameziburuza mahakamani, Tume ya Utumishi wa Mahakama (JSC) na Kamati ya Maadili ya Maafisa wa Mahakama (JOEC), kwa kumfuta kazi.

Mgongoro, alifutwa kazi na Tume ya Utumishi wa Mahakama, Julai 17 mwaka huu, kutokana na ushauri wa Kamati ya Maadili ya Maafisa wa Mahakama, kutokana na tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa.

JSC inaongozwa n Jaji Mkuu wa Tanzania, ambaye ni mwenyekiti na katibu wake ni mtendaji mkuu wa mahakama, huku mwenyekiti wa JOEC akiwa ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu na katibu wake ni Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Hata hivyo, Oktoba 17, mwaka huu, hakimu Mgongoro alifungua shauri rasmi Mahakama Kuu, dhidi ya JOEC, JSC na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ambalo lilisajiliwa rasmi mahakamani hapo Oktoba 30, mwaka huu na kupewa namba ya usajili namba 28 la mwaka 2019.

Kabla ya kufungua shauri hilo, Septemba 23 mwaka huu, Hakimu Mgongoro alifungua maombi mahakamani hapo akiomba kibali cha kufungua shauri hilo na Oktoba 10 mwaka huu, mahakama hiyo ilimkubalia na kumruhusu kufungua shauri hilo.

Katika hati ya maombi ya shauri hilo, Hakimu Mgongoro anaiomba mahakama hiyo itoe amri ya kutengua uamuzi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, uliomo katika barua ya Julai 17, mwaka huu wa kumfuta kazi.

Advertisement

Katika hati ya kiapo chake kinachounga mkono maombi hayo pamoja na hati ya maelezo yake anadai kuwa amekuwa mwajiriwa wa Mahakama tangu Februari Mosi mwaka 2001, hadi tarehe aliyofutwa kazi.

Anadai kuwa alifanya kazi kwa uadilifu na weledi, huku akiwa na kumbukumbu nzuri, ambapo alipanda vyeo hadi kufikia cheo cha Hakimu Mkazi Mwandamizi baada ya kufanya kazi katika mahakama za wilaya mbalimbali.

Hata hivyo, anadai kuwa Machi 28, 2017, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, kwa maelekezo ya Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, alimsimamisha kazi.

Anadai kuwa barua hiyo ilieleza kuwa Kaimu Jaji Mkuu amepokea malalamiko ya rushwa dhidi yake na kwamba alikuwa na nyaraka zote za ushahidi, lakini barua hiyo haikutaja wala kuainisha mlalamikaji wala mtu aliyewasilisha malalamiko hayo.

Hakimu Mgongoro anadai kuwa Novemba 15, 2017 alipokea barua kutoka JOEC ikimfahamisha kwamba Tume ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imefungua malalamiko dhidi yake na kwamba JOEC imeamua kumshtaki kwa mwenendo mbaya.

Advertisement