VIDEO: Halima Mdee, Bulaya wapambana kutofutiwa dhamana

Muktasari:

Wabunge wa Chadema, Halima Mdee na Ester Bulaya leo Jumanne Januari 21, 2020  wameeleza kwa nini Mahakama ya Hakimu Mkazi isiwafutie dhamana.

Dar es Salaam. Wabunge wa Chadema, Halima Mdee na Ester Bulaya leo Jumanne Januari 21, 2020  wameeleza kwa nini Mahakama ya Hakimu Mkazi isiwafutie dhamana.

Uamuzi iwapo watafutiwa dhamana au la utatolewa Januari 31, 2020 na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Hata hivyo, kesi itaendelea kusikilizwa kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa utetezi Januari 22,23 na 24, 2020.

Wabunge hao wa Kawe na Bunda jana Julai 20, 2020 walitakiwa kujieleza kwa nini wasifutiwe dhamana baada ya wakili wa Serikali mkuu, Faraja  Nchimbi kuibua hoja kuwa walipata taarifa kupitia vyombo vya Dola kuwa washtakiwa hao walionekana wakiingia nchini wakitokea nje ya nchi.

Kutokana na hali hiyo Nchimbi amedai miongoni mwa masharti ya dhamana katika kesi namba 112/2018 inayowakabili washtakiwa hao na wenzao saba ni kutosafiri nje ya nchi bila kuwa na kibali cha mahakama.

Aliomba washtakiwa hao wajieleze kwa nini wasifutiwe dhamana kwa kusafiri nje ya nchi bila ya kuwa na kibali cha mahakama huku wadhamini wao pia wakitakiwa kujieleza kwa nini wasiondolewe kuwadhamini washtakiwa hao kwa kuvunja masharti ya dhamana.

Leo washtakiwa na wadhamini wao wamejieleza mbele ya Hakimu Simba kwa nini wasifutiwe dhamana zao.

Wamekiri kwenda Afrika Kusini, Bulaya akieleza kuwa alimsindikiza Mdee katika matibabu.

Washtakiwa hao na wenzao saba wanakabiliwa na mashtaka 13 ikiwemo kula njama,  kufanya mkusanyiko wenye ghasia,  kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika na uchochezi makosa yanayodaiwa kutendeka kati ya Februari Mosi na 16, 2018  jijini Dar es Salaam.

Alichokisema Mdee

Akizungumza kwa nini asifutiwe dhamana, Mdee amesema hakuwa na dhamira ya kuidharau mahakama.

Mbunge huyo wa Kawe ambaye kitaaluma ni mwanasheria amesema hata yeye ni ofisa wa mahakama, kwamba hali yake ya afya inafahamika na amekuwa akishindwa kufika mahakamani.

Amesema ana kesi mbili mahakamani hapo,na zote zinasikilizwa na hakimu mmoja, alitambua kuwa hali yake ya ugonjwa inaweza kuathiri ushiriki wake katika kesi hizo.

Amebainisha kuwa kabla ya kusafiri alijiridhisha kupitia wakili wake, kuwasilisha nyaraka za safari ikiwamo hati yake ya kusafiria.

"Ukiangalia barua ya daktari nilitakiwa nikae zaidi lakini kwa kuzingatia umuhimu wa kesi hii nimelazimika kurejea mapema zaidi ili niweze kuwa mahakamani,” amesema Mdee.

Maelezo ya Bulaya

Kwa upande wake Bulaya amedai hawezi kuidharau mahakama wala kukiuka masharti ya dhamana na ndio maana amekuwa akihakikisha mdhamini wake anakuwepo mahakamani siku ambazo anakuwa na udhuru.

“Mahakama inafahamu afya ya Mdee na matibabu yake,  mama yake (mama yake Mdee) ni mtu mzima na ni mtoto wa kike pekee kwenye familia yao kama mwanamke mwenzie nilimsindikiza kupata matibabu,” amesema Bulaya.

Wakili wa Serikali ataka dhamana kufutwa

Baada ya maelezo hayo wakili wa Serikali, Faraja Nchimbi amesema washtakiwa wamekiuka sharti la dhamana la kutotoka nje ya Tanzania bila kibali cha mahakama.

“Kwa kuwa walivunja masharti ya dhamana na ni mara ya pili uzingatiaji wao wa masharti ya dhamana unatia wasiwasi tunaiomba mahakama kutengua dhamana zao,” amesema Nchimbi.

Wakili huyo amedai iwapo mahakama itaona hoja zao hazijitoshelezi itoe amri ya kushikilia hati za kusafiria na kuzihifadhi katika mahakama hiyo.

Ametaka mahakama hiyo kutoa onyo kwa washtakiwa hao ili iwe kumbukumbu kwa washtakiwa wengine kutofanya kosa kama hilo.

Hakimu Simba amesema shauri hilo tangu lilipokuwa likiendeshwa na hakimu Wilbroad Mashauri ambaye kwa sasa ni Jaji, kwa muda wa mwaka mmoja na nusu nguvu nyingi zimetumika katika dhamana.

Hakimu huyo ameahirsha kesi hiyo hadi Januari 31, 2020 kwa ajili ya uamuzi na kuanzia kesho kesi hiyo  itaendelea na usikilizwaji wa ushahidi wa upande wa utetezi hadi Januari 24.

Novemba 21, 2019 Mdee na Bulaya pamoja na washtakiwa wenzao, mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa na mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche walinusurika kufutiwa dhamana baada ya kukiuka masharti ya dhamana kwa kutofika mahakamani bila ya kutoa taarifa yoyote.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe; mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko; katibu mkuu wa Chadema, John Mnyika; naibu katibu mkuu wa chama hicho, Salum Mwalimu na Dk Vicent Mashinji.