VIDEO: Halima Mdee alivyozungumzia amani, mikutano ya hadhara Tanzania

Muktasari:

  • Baraza la wanawake Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bawacha) nchini Tanzania limeelezea mikakati yake ya mwaka 2020 ikiwamo kuzunguka nchi nzima kuzungumza na wanawake pamoja na kuhamasisha amani.

Dar es Salaam. Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bawacha) nchini Tanzania limesema limejipanga kikamilifu kuhakikisha amani ya nchi inadumishwa na kuondoa tamaduni ambazo zimejengeka kimazoea.

Akizungumza leo Jumatano Januari 8, 2020 katika mkutano wake na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Bawacha, Halima Mdee amesema baraza hilo limeazimia kuwa haki, demokrasia na amani ya wananchi inadumishwa.

Amesema tamaduni za kimazoea kama watu kupigwa risasi, kubambikiwa kesi na kukandamiza haki za raia zinachafua nchi hivyo wamesema watasimama kuhakikisha tamaduni hizo zinaisha.

“Tunataka nchi hii iwe na amani na jukumu la kuileta amani ni sisi Watanzania, watu wamejaa hofu wanashindwa kuhoji, wanashindwa kuongea, wanashindwa kujitetea kwa sababu hakuna wa kusimama na kuirejesha amani hii iliyopotea,” amesema Mdee ambaye pia ni Mbunge wa Kawe.

Amesema baraza hilo litakuwa chachu ya mabadiliko kwa viongozi na mabaraza mengine katika kuhakikisha haki ya mwanamke inalindwa.

Katika mkutano huo, Mdee amesema baraza hilo litazunguka katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania kutoa elimu kwa wananchi kuhusu amani ambayo wamenyimwa huku wakijua ni haki yao ya msingi.

“Tuliambiwa kuwa mwaka huu 2020 ndiyo mwaka ambao Rais John Magufuli alisema ataruhusu mikutano ya kisiasa kwa hiyo wakati ndiyo huu tutazungumza na wananchi bila hofu yoyote lengo ni kuonana na wanawake wenzetu kusikiliza changamoto zao kwa sababu mwanamke ana nafasi kubwa katika maendeleo ya taifa hili,” amesema.