Hamahama ya makatibu wa Chadema yaibua hisia tofauti

Chadema, ambacho ni chama kikuu cha upinzani nchini, wiki hii kimepata pigo baada ya kuondokewa na aliyekuwa katibu wake mkuu, Dk Vincent Mashinji, aliyehamia CCM.

Mashinji anakuwa mmoja wa viongozi wa juu wa Chadema kuondoka na wote kujiunga na CCM katika kipindi cha kuanzia mwaka 2015.

Wengi wa wanachama hao walioondoka ni wale waliojiunga Chadema wakitoka CCM, hasa wakati wa kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 uliokuwa na msisimko mkubwa.

Dk Mashinji anakuwa mtu wa pili aliyewahi kushika nafasi hiyo nyeti ya mtendaji mkuu wa Chadema kuondoka na kujiunga na CCM tangu mwaka 2015, na wa tatu wa nafasi hiyo tangu kurejeshwa kwa siasa za vyama vingi.

Wengine walioondoka kabla ni Dk Wilibroad Slaa, ambaye alijivua nafasi zote na uanachama wa Chadema akipingana na uamuzi wa kumpa Edward Lowassa, ambaye pia alitokea CCM, nafasi ya kugombea urais mwaka 2015.

Mbali na Dk Slaa, ambaye aligombea urais kwa tiketi ya chama hicho mwaka 2010, mwingine ni Dk Walidi Kabourou.

Dk Mashinji pia amekuwa kiongozi wa nne wa chama hicho kuhama ndani ya kipindi kifupi. Wengine walioondoka ni mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Fredrick Sumaye na aliyekuwa mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe.

Hata hivyo, wakati Mashinji akitangaza kuondoka ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini alikuwa mwanachama wa kawaida, kwa kuwa alishaanguka katika uchaguzi wa mwenyekiti wa Kanda ya Kusini na juhudi zake za kuwania uenyekiti wa chama hicho ziliisha vibaya.

Tayari chama hicho kimeshasema kuwa hakijastushwa na uamuzi huo wa Dk Mashinji kwa kuwa kilishajua mipango yake na watu wengine ambao

Inaendelea uk 22

Inatoka uk 21

chama hicho kilidai walikuwa na mapngo mmoja wa kuchukua madaraka ya Chadema kw alengo maalumu.

Dk Mashinji hakupendekezwa tena na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuendelea na wadhifa huo na ilionekana dhahiri ukumbini kutokana na shamrashamra za wajumbe wa mkutano mkuu baada ya John Mnyika kupendekezwa kuwa katibu mkuu.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema kitendo cha viongozi hao kuhama Chadema kinawafanya wasiaminike tena kwa wananchi na pia ni hatari kwa mustakabari wa vyama vya upinzani hasa ikizingatiwa walikuwa wakiingia katika vikao vya juu vya maamuzi.

“Kwa kawaida, wanasiasa si watu wa kuwaamini kwa kuwa hubadilika kulingana na mazingira au muda,” anasema mhadhili wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI), Dk Jimson Sanga anasema.

Anasema Chadema kwa sababu ndio chama kikuu cha upinzani ni rahisi viongozi wake kama makatibu wakuu kuhamia chama kingine hasa CCM kunapotokea kutoelewana.

“Na sababu kubwa ni wao huko ndani kutoelewana. Kama wakielewana na kukiwa na misingi ya uongozi kama ilivyo kwa CCM sio rahisi vigogo hasa makatibu kuondoka,” anasema Dk Sanga.

“Anapohama kigogo hata siri za vikao haziwezi kutunzika, lazima ulioutumia upande wa kwanza atautumia upande mwingine.”

Lakini kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe anasema viongozi hao kuhama ni haki yao kwa kuwa wametekeleza takwa la kikatiba.

“Sasa anachosema baada ya kutoka chama kimoja kwenda chama kingine, huo ni mjadala na kila mtu ana tafsiri yake,” alisema Zitto, ambaye pia alikuwa naibu katibu mkuu wa Chadema kabla ya kuhamia ACT-Wazalendo na nafasi yake kuchukuliwa na Mnyika.

“Lakini jambo ambalo nataka kukubaliana na watu wengi ni kwamba kitendo cha madiwani, wabunge na viongozi wa ngazi ya kitaifa ya vyama kutoka upinzani kwenda CCM kinawavunja nguvu wananchi.

“Ni kitendo ambacho kinaweka mashaka katika imani ya wananchi kwa wanasiasa. Hivyo sisi tuliobaki tuna kazi kubwa ya kuwaonyesha wananchi kwamba tunaendelea na mapambano,” alisema.

Kuhama kwa Dk Mashinji na viongozi wengine pia kuliibua mjadala mitandaoni ambako wengi walikosoa kitendo hicho.

“Chadema haina sababu ya kujiuliza tatizo lao hawa makatibu wastaafu,” ameandika mtu anayejiita Deograties katika akaunti yake ya Twitter.

“Wakikosa nafasi, wanakimbia ila wakiwa nazo wanakaa. It is matter of interest (ni suala la maslahi) tu hamna cha maana.”

Mtu mwingine anayejiita Zeela Ndefu ameandika: “Katika kitu wanachofeli Chadema ni kudharau wanachoambiwa au kukosolewa. Nadhani kuna mengi yanakuja ndio wataelewa kwanini watu waliwapa tahadhari. Hatutaki kuambiwa ukweli bali tunapenda kusifiwa tu na haya ndio madhara yake.”

Chadema ilivuna wanachama wengi wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015, na hasa baada ya Lowassa, ambaye alikuwa waziri mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne, alipojiunga na chama hicho na kupewa nafasi ya kugombea urais.

Lowassa alifuatwa na wabunge, wenyeviti wa mikoa, madiwani na wenyeviti was serikali za mitaa na kuiwezesha Chadema kuingiza wabunge zaidi bungeni, kushika mitaa kadhaa na kuongeza idadi ya madiwani huku mgombea wake wa urais akivuna kura milioni 6.07, ambayo ni idadi kubwa tangu uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi wa mwaka 1995.

Chadema ilianza kupoteza waliokuwa viongozi wake wa juu mwaka 2006 wakati Dk Walid Kabourou (marehemu) alipotangaza kujiunga na CCM kwa maelezo ya kuvutiwa na ilani ya uchaguzi ambayo alisema inatekelezeka.

Dk Kaborou, ambaye wakati huo alikuwa makamu mwenyekiti wa Chadema, alisema aliamua kwa hiari yake bila kulazimishwa na mtu yeyote kurudi CCM.

Baadaye Zitto, aliyekuwa naibu katibu mkuu Bara, alitimuliwa na vikao vya chama hicho baada ya kutuhumiwa kutaka kufanya mapinduzi. Hata hivyo, kesi aliyofungua ilisababisha abakie ndani ya chama na ubunge wake hadi mwaka 2010.

Katika kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015, ilikuwa zamu ya Dk Slaa baada ya ujio wa Lowassa. Aliondoka nchini na kwenda barani Ulaya na baadaye akateuliwa kuwa balozi.

Dk Slaa alisema anaachana na siasa, baada ya kuona misingi ya chama alichoshiriki kukijenga imepotoshwa.

Na juzi ilikuwa zamu ya Dk Mashinji aliyekituhumu chama hicho kuwa ni mali ya mtu binafsi na hakiendani na itikadi yake. Alidai hakuna uwazi wa mapato na matumizi, madeni ya chama, ruzuku na mapato mengine.

Kiongozi huyo aliibuliwa na Mbowe katika siasa ndani ya chama hicho wakati wa mkutano wa baraza kuu la taifa lililofanyika mkoani Mwanza, huku baadhi ya wajumbe wakipinga pendekezo hilo la Mbowe.