UTATA: Hapa ndipo fedha kwenye simu ya mtu aliyekufa zinapokwenda

Muktasari:

Kwa miaka 10 ya kuwapo kwa huduma za fedha kupitia simu za mkononi, taarifa za Jeshi la Polisi zinaonyesha kulikuwa na ajali 37,421. Ajali hizo zilizotokea kati ya mwaka 2009 hadi 2018 ambazo ni wastani wa 10 kila siku zilisababisha vifo 8,004.

Ajali na majanga mengine ni miongoni mwa vyanzo vya vifo vya ghafla ambavyo huwakumba wateja wa simu za mkononi na hakuna mtu mwingine mwenye uwezo wa (kujua namba za siri) kufikia akiba iliyoachwa.

Dar es Salaam. Watu wengi nchini siku hizi wanatumia simu za mkononi si kwa kuwasiliana tu, bali pia kuweka na kutuma fedha. Ili kuzifikia fedha hizo kunahitajika namba ya siri. Je, umeshawahi kujiuliza watu wanaokufa wakiwa na fedha kwenye simu zao au kupatwa na majanga mengine, amana zao zinakwenda wapi?

Mara nyingi wasimamizi wa mirathi husahau kufuatilia salio lililomo kwenye akaunti hizo hivyo kupoteza mamilioni ya fedha.

Elizabeth George, mkazi wa jijini hapa anasema isingekuwa kufahamiana kwake na hakimu wa mahakama aliyofuatilia mirathi ya kaka yake aliyefariki ghafla mkoani Mbeya, akiba iliyokuwamo kwenye simu za marehemu ingepotea.

“Kaka alifariki ghafla. Baada ya mazishi wifi akateuliwa kusimamia mirathi. Nilimsindikiza mahakamani kwenda kusajili kwa sababu nilikuwa nafahamiana na hakimu. Huyo hakimu alituuliza kama marehemu alikuwa na simu na tumeangalia salio lililomo,” alisema Elizabeth.

Hawakuwa na wazo hilo na wifi yake hakuwa anajua namba za siri za simu zote tatu za mumewe. Waliandikisha na wifi yake akafuatilia kwenye kampuni zote tatu ambazo zilikuwa ni Mpesa, Tigopesa na Airtel Money.

Baada ya kufuatilia, anasema walikuta Sh2 milioni kwenye akaunti ya Mpesa, Sh1.5 milioni kwenye Airtel Money na Sh980,000 kwenye Tigopesa. “Tusingekumbushwa, fedha hizi zingepotea,” alisema Elizabeth.

Tangu simu za mkononi zilipoanza kutoa huduma za fedha, muongo takriban mmoja uliopita, hadi Desemba 2018, taarifa za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha kulikuwa na watumiaji milioni 23.3 kati ya watumiaji milioni 43.6 wa simu za mkononi waliosajiliwa.

Wengi wa wateja hao wamekuwa wakisahau kujumuisha akiba iliyomo kwenye simu za mkononi hivyo Serikali kukusanya mapato hayo kwa kipengele cha mali isiyo na mwenyewe.

Mkurugenzi wa usimamizi wa mashauri ya Mahakama Tanzania, Eva Nkya alisema suala la kuainisha mali na madeni ya marehemu hufanywa katika kikao cha familia kabla ya kusajili mirathi husika mahakamani. Kazi kubwa ya msimamizi wa mirathi ni kufanya uchunguzi wa kutosha ili kukusanya mali zote katika akaunti za benki na simu za mkononi, hisa za kampuni, riba za mikopo aliyokopesha, pensheni na bima, kisha kulipa madeni ya marehemu na kugawa mali kwa warithi.

“Sheria inampa msimamizi wa mirathi muda wa kutosha kukusanya mali, kuzigawa na kulipa madeni kama yapo na mwisho mirathi kufungwa. Kwa mahakama za mwanzo, msimamizi hupewa miezi minne na kwingine ni miezi sita,” alisema Eva.

Akaunti ya simu

Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa Umma wa kampuni ya Tigo, William Mpinga alisema kuna sababu kadhaa za kuzingatia kabla ya kufunga akaunti iliyotelekezwa ya Tigopesa.

Sababu hizo alisema ni kutotumika kwa akaunti husika kwa walau miezi sita akisema itakufa kabisa endapo namba haitopiga simu, kutumika kwenye data, kutuma ujumbe mfupi wa maneno au kuongeza salio kwa miezi mitatu au zaidi.

Sababu nyingine ni akaunti kuhusika katika uhalifu, mteja mwenye akaunti kufariki na taarifa zake kuwasilishwa Tigo. “Hata mamlaka kama TCRA, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) au vyombo vya sheria vikitoa agizo namba na akaunti hiyo hufungwa.”

Kwa mteja ambaye akaunti haijafanya kazi kwa miezi sita na zaidi au mteja mwenye akaunti amefariki na taarifa kuwasilishwa Tigo, Mpinga alisema, “akiba iliyokuwamo hurudishwa.”

Aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa Vodacom, Ian Ferrao aliwahi kuliambia gazeti hili kuwa akaunti ya mteja wa M-Pesa huendelea kuwa hai kwa siku 270 na baada ya hapo salio lililopo huhamishiwa BoT na akaunti kufungwa kwa mujibu wa sheria lakini mteja akijitokeza, salio lake hurudishwa.

Kampuni za simu hutunza fedha kwenye akaunti ya benki ijulikanayo kama Akaunti ya Trust na inapotokea mteja hajatumia akaunti yake ya simu kwa muda mrefu iwe kutokana na kifo, kusafiri nje ya nchi, kufungwa gerezani au kuugua, salio lake huhamishiwa BoT.

Zinapohamishiwa BoT, Mkurugenzi wa Mifumo ya Malipo ya Taifa, Bernard Dadi alisema hutunzwa kwa kuzingatia (Sheria ya Mali Isiyo na Mwenyewe) Unclaimed Property Act.

Huduma za fedha kwa simu za mkononi, zinasimamiwa na kifungu cha 31 cha Kanuni za Fedha za Miamala za mwaka 2015. Endapo mteja husika hatajitokeza kwa muda muafaka (kati ya miezi sita hadi tisa kutegemea na kampuni ya simu), fedha hizo huhamishiwa serikalini.

Kwa mujibu wa kanuni hizo, kigezo kikubwa kinachozingatiwa kuifanya akaunti ionekane imetelekezwa, Dadi alisema ni ukomo wa miaka mitano ya mwenye akaunti kutojitokeza.

Muda huo ukipita, BoT huzipeleka fedha husika kwa Msajili wa Hazina baada ya kuzipokea kutoka kwa watoa huduma. Lakini, endapo mteja wa akaunti atapatikana au mrithi wake kujitokeza na kukamilisha utaratibu wa mirathi, basi kampuni ya simu humsaidia kuzipata fedha za marehemu.

“Asipojitokeza kwa miaka 15 Serikali huzitumia,” alifafanua.

Akaunti za benki

Utaratibu wa kutambua na kukusanya mali isiyo na mwenyewe pia hutumika kwenye akaunti za benki ambako mteja asiyeitumia akaunti yake kwa miaka 15 mfululizo, salio lake huhamishiwa BoT.

Mteja wa akaunti au mali iliyohifadhiwa benki asipoonekana kwa muda huo, Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha inaagiza akiba iliyomo au mali husika iliyohifadhiwa kuhesabiwa kama iliyotelekezwa.

Baada ya miaka 15 ya fedha hizo kutunzwa BoT, hupelekwa serikalini na kupangiwa matumizi kwa mujibu wa sheria.